Vivumishi au visifa ni maneno yanayotuelezea zaidi kuhusu nomino. Aghalabu vivumishi hutanguliwa na
nomino. kuna aina kumi na moja za vivumishi, navyo ni;

  1. Vivumishi vya Sifa
  2. Vivumishi Vimilikishi
  3. Vivumishi vya Idadi
  4. Vivumishi Visisitizi
  5. Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
  6. Viwakilishi Viulizi
  7. Vivumishi Virejeshi
  8. Vivumishi vya KI-Mfanano
  9. Vivumishi Vya A-Unganifu
  10. Vivumishi vya nomino/jina
  11. Vivumishi vya pekee

Vivumishi vya Sifa
Hivi ni vivumishi ambavyo hutoa sifa ya kitu, mtu, mahali, n.k
k.m: kizuri, kali, safi, mrembo
Yule mama mweusi hupika chakula kitamu.
Mvulana mkorofi aliadhibiwa na mwalimu kutokana na tabia zake mbaya.
Sauti nzuri humtoa nyoka mkali pangoni
Vivumishi Vimilikishi
Vivumishi hivi hutumika kuonyesha nomino inamiliki nyingine. Mizizi ya vivumishi hivi
huundwa kulingana na nafsi mbalimbali ( -angu, -ako, -ake, -etu, -enu, -ao).
k.m: changu, lako, yake, kwetu, vyenu, zao
Nitatumia talanta zangu kwa manufaa ya taifa letu.
Aliweka kitabu chako sebuleni mwako
Katosha amepata nguo yake miongoni katika sanduku lao.
Vivumishi vya Idadi
Hutueleza zaidi kuhusu kiasi, au idadi ya nomino. Kuna aina mbili za vivumishi vya idadi.
a) Vivumishi vya idadi Kamili- hutumia nambari kuelezea idadi ya nomino.
k.m: tatu, mbili, kumi
Msichana mmoja amewauwa nyoka wawili
Siku kumi zimepita tangu Bi Safina alipojifungua watoto watatu
b)Vivumishi vya idadi Isiyodhihirika- huelezea kiasi cha nomino kwa ujumla, bila kutaja idadi kamili
k.m: chache, nyingi, kadhaa, kidogo, wastani
Watu wachache waliohudhuria mazishi ya Kajuta walikula chakula kingi sana.

Baba yao alikuwa mateka kwa miaka kadhaa.
Vivumishi Visisitizi
Husisitiza nomino fulani kwa kurudia rudia kivumishi kiashiria.k.m: yuyu huyu, wawa hawa, kiki hiki, papo hapo, mumu humu,
Jahazi lili hili

Wembe ule ule
Ng’ombe wawa hawa
Vivumishi Viashiria / Vionyeshi
Vivumishi viashiria hutumika kuonyesha au kuashiria nomino kulingana na mahali.

k.m: Karibu – hapa, huyu, hiki, hili, huku, haya, ule, wale, pale
Mbali kidogo – hapo, huyo, hiyo, hicho
Mbali zaidi- pale, lile, kile,
Msichana huyu ni mkubwa kuliko yule
Jani hili la mwembe limekauka
Tupa mpira huo
Viwakilishi Viulizi
Vivumishi viulizi hutumika kuuliza swali.
Baadhi ya vivumishi viulizi huchukua viambishi vya ngeli
k.m: -ngapi?, -pi?
Ni walimu wangapi wamefukuzwa? – kuulizia idadi
Je, ni dawati lipi lenye funguo zangu?
Kunavyo vivumishi viulizi vingine ambavyo havichukui viambishi vyovyote.
k.m: wapi?, gani?, nini?, vipi?
Unazungumza kuhusu kipindi gani?
Je, mmefika mahali wapi? – kuulizia mahali

Vivumishi Virejeshi
Hivi ni vivumishi ambavyo hurejelea nomino. Vivumishi hivi vinaweza kuwa vivumishi vya O-
rejeshi au vivumishi viashiria vinapotumika kurejelea nomino.
k.m: ambaye, ambao, ambalo, ambacho,
Msichana ambaye alikuja ni Sheila
Sauti ambayo uliisikia ilikuwa ya Mzee Kasorogan
Vivumishi vya KI-Mfanano

Vivumishi vya KI- ya Mfanano hutumika kulinganisha sifa ya nomino na hali au tabia nyingine.
Vivumishi hivi hutanguliwa na nomino, kiunganishi cha A-unganifu na huchukua kiungo KI.
k.m: wa kifalme, za kijeshi, ya kitajiri, n.k
Chifu wa Vikwazoni anaishi maisha ya kimasikini
Chali anapenda kusikiliza mziki wa kizungu
Bi Naliza huvulia mavazi ya kifalme.
Vivumishi Vya A-Unganifu
Vivumishi hivi hutuelezea zaidi kuhusu nomino kwa kuonyesha kitu kinachomiliki nomino hiyo.
Huundwa kwa kuambatanisha kiambishi cha nafsi/ngeli pamoja na kiambishi -a cha a-unganifu,
kisha nomino
k.m: cha, la, kwa, za, ya
Watoto wa mwalimu mkuu wana tabia nzuri
Chai ya daktari imemwagika

Vivumishi vya nomino/jina

Kivumishi cha nomino ni nomino inayotumiwa kutoa taarifa zaidi kuhusu nomino nyingine.mara nyingi hutokea wakati nomino mbili hufuatana katika sentensi.

k.m mzee mrogi ameteketezwa

mtoto mvulana amezaliwa jana

Askari jeshi amekamata mwizi

Vivumishi vya pekee

Vivumishi vya pekee husimamia nomino kwa kuonyesha upekee wake. vivumishi hivi husimamiwa na na mizizi ifuatayo:

MziziMaana
-enyekumiliki/Umilikisho
-enyeweBila kusaidiwa
-o-oteBila kuchagua/kubagua
-oteBila kusaza/ bila kubakisha
ingineSehemu ya/Zaidi ya/tofauti na
ingineoZaidi ya/ dhana ya ziada
mifano katika sentensi;

Niletee maziwa mengine

Chakula chote kimeliwa

Mgonjwa yeyote atahudumiwa

Mtu mwenye macho haambiwi tazama

Aina za Maneno
Nomino-N
Kiwakilishi-W
Kitenzi-T, Ts au t
Kiunganishi – U
Kihusishi – H
Kihisishi – I