Mfasiri katika kazi yake ya kufasiri hukumbana na changamoto mbalimbali, ambazo huweza kusababisha tafsiri kuwa na mapungufu ya hapa na pale. Baadhi ya changamoto au mapungufu hayo ni kama vile:
(i) Tofauti za kiisimu kati ya lugha chanzi na lugha lengwa.
Tofautui za maumbo, miundo na maana kati ya lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza wakati mwingine husababisha matatizo au upungufu katika tafsiri na ukalimani. Kwa mfano maumbo ya vitenzi vya Kiingereza huruhusu kauli nyingi elekezi kutoonesha umoja au wingi wa wahusika wala majina ya vitu mahususi vinavyoambatana na maelekezo yanayotolewa tofauti maumbo ya vitenzi vya Kiswahili ambavyo huonesha umoja na wingi wa wahusika na hata kuwa na majina ya vitu husika, tazama mifano ifuatayo kama ilivyotolewa na, Mwansoko [2006]
Kingereza Kiswahili
No parking ? Usiegeshe gari hapa [je kisichoruhusiwa kuegeshwa ni gari tu?]
No Smoking ? Usivute sigara[ Je ni sigara tundiyo hairuhusiwi kuvutwa?]
Arrivals ? Wanaowasili
Departures ? Wanaosafiri
Vilevile tofauti za maana kati ya lugha ya Kingereza na Kiswahili huweza kuathiri tafsiri au ukalimani, mathalani:
Kiswahili Kingereza
Wasiojiweza ? Disabled [Siyo wote wasiojiweza ni walemavu]
[na siyo walimavu wote hawajiwezi]
Wezi wa mifukoni? Pickpockets [Hawaibi kwenye mifuko, wanaiba kutoka mifukoni]
(ii) Tofauti za mitindo kati lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti za mitindo ya uzungumzaji pia, huweza kuathiri tafsiri na ukalimani na hii ni kwa sababu unaweza kukuta kuna mitindo fulani inaweza kutumika katika muktadha fulani lakini ikishindwa kupata tafsiri katika lugha nyingine katika muktadha ule ule.mathalani:
Kingereza: Kiswahili
(i) Thou shalt not steal [mtindo wa kidini] ? Usiibe
Do not steal [mtindo wa kawaida] ? Usiibe
(ii) Lend me your ears [mtindo wa kishairi] ? Naomba mnisikilize
May I have your attention [kawaida] ? Naomba mnisikilize
Tafsiri zote tulizoziangalia katika mfano wa (i) na (ii) zimetoa maana au taarifa ili ile iliyomo katika matini chanzi lakini tafsiri hizo hazikuzingatia mtindo wa lugha iliyotumika katika matini chanzi.
(iii) Tofauti za kitamaduni kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti za kiutamaduni, yaani taofauti za kimila, desturi na mazingira ya watumiaji wa lugha chanzi na lugha lengwa huweza kufanya tafsiri au ukalimani kuwa mgumu, kwa mfano, katika utamaduni wa Waingereza wana milo minne wakati Waswahili wana milo mitatu na hii hupelekea kuwa vigumu kupata dhana za milo ya hiyo ya Waingereza katika dhana ya Kiswahili. Mfano:
Waingereza wana: Waswahili wana:
Breakfast —————— Kifungua kinywa
Lunch …………………… Chakula cha mchana
High tea ……………………?
Dinner ……………………Chakula cha jioni
Supper …………………….?
Kwa hiyo ukiangalia mifano hiyo, utaona kuwa, high tea na supper kuzipata dhana zake katika lugha ya Kiswahili ni ngumu kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kuwa na milo kama hiyo kwa siku. Lakini pia inakuwa vigumu kupata tafsiri ya vyakula kama vile ugali, makande katika lugha ya Kiingereza kutokana na kutokuwa na vyakula vya aina hiyo.
(iv) Tofauti za kiitikadi kati ya lugha chanzi na lugha lengwa
Tofauti za kiitikadi pia huweza kuathiri tafsiri na ukalimani, na hii ni kwa sababu, utakuta wafasiri wengi hususani waandishi wa habari kuegemea katika itikadi zaidi, kwa mfano:
Kingereza Kiswahili
Bussnessman ? mlanguzi [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na itikadi
ya ujamaa]
mfanyabiashara [tafsiri hii inatokana mfasiri kuathiriwa na
itikadi ya ubepari]
Freedom fighter ? wapigania uhuru [Tafsiri ya vyombo vya habari vya
Tanzania wakati wa kupigania uhuru]
Magaidi [Tafsiri ya idhaa ya BBC na Radio za Afrika
Kusini wakati huo]
Hivyo basi kwa kuhitimisha tunaweza kusema kuwa, ukalimani mzuri unawezekana kwa kiwango ambacho mila na desturi zote yaana za lugha chanzi na lugha lengwa zinalingana ama kushabihiana.
Na kutokana na umuhimu wa taaluma hii ya tafsiri na ukalimani, serikali kupitia Baraza la Kiswahili la Taifa Bakita [BAKITA] imeanzisha idara maalumu ya Tafsiri na Ukalimani, na idara hiyo ina majukumu yafuatayo:
- Kutoa huduma za tafsiri na ukalimani kwa lugha mbalimbali kwa masharika, idara, wizara, balozi na watu binafsi.
- Kuratibu na kutoa huduma za ukalimani kwenye mikutano ya kitaifa na kimataifa na katika shughuli za masharika, makampuni na watu binafsi.
- Kupitia na kuthibitisha tafsiri zilizofanywa na asasi mbalimbali au wafasiri wa nje.
- Kutoa ushauri kuhusu masula ya tafsiri na ukalimani.
MAREJEO
Cartford [1995] A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press
Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.
Oxford University Press Dar-es-salaam
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.
D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2018
www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2018
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2018
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman