Changamoto zinazomkumba mtafiti katika utafiti nyanjani

Utafiti ni shughuli ya kitaalamu  ya kutafuta habari.Habari hizi zinaweza zikatafutwa
miongoni mwa  watu,vitabu,magazeti, nyanjani, majarida na mtandaoni.Utafiti hufanywa  ikiwa kuna tatizo  ambalo linahitaji suluhisho au kuna jambo lisiloeleweka.

Utafiti hujishughulisha na  ukusanyaji wa data  kwa kuzingatia utaratibu maalum kwa lengo la kutaka kutatua tatizo  Fulani la kitaalamu,au kujaliza  pengo katika kazi ya wataalamu wa hapo awali ambao hawakuzungumzia dhana Fulani kwa ukamilifu
wake.Kuna aina nyingi za utafiti lakini kazi hii itajikita katika utafiti nyanjani.Utafiti nyanjani ni utafiti ambo  mtafiti anakwenda nyanjani ili aweze kukusanya data ambayo itatumika katika  kutatua tatizo lake analolitafitia.Ni utafiti ambao jibu la tatizo hupatikana nje ya maktaba hivyo kumlazimu mtafiti  kuzuru nyanjani kutafuta data.Mtafiti huweza kuipata data kwa kutangamana na jumuiya kwa kuihoji,kuchunguza tabia au kufanya kesi stadi  ya elementi mbalimbali.

Kazi hii imegawika katika sehemu kuu mbili.Katika sehemu ya kwanza,kazi  hii itashughulikia  baadhi ya  changamoto ambazo watafiti hukumbana nazo nyanjani na mbinu ambazomtafiti anaweza kuzitumia katika kusuluhisha changamoto hizo.

 Changamoto zinazomkumba mtafiti nyanjani ni yale matatizo ambayo mtafiti hukumbana nayo katika
kukusanya data nyanjani.Hii inaweza kuwa ule ugumu wa kupata data lengwa ,mtafiti kuathirika kiafya  au kisaikolojia
kutokana na shughuli ya utafiti wenyewe. Kila changamoto itazungumziwa kwa undani jinsi inavyoweza kumwathiri mtafiti nyanjani na kisha pendekezo kutolewa mwishoni jinsi ambavyo mtafiti anaweza akakabili changamoto hizo ambazo zinawezamkumba nyanjani.

 Katika sehemu ya pili kazi hii  itachunguza manufaa na matatizo ya vifaa viwili vya utafiti.Vifaa vya utafiti ni nyenzo ambazo mtafiti huzitumia katika ukusanyaji wa data  kutoka kwa jumuiya. Ili mtafiti aweze kufanikiwa katika utafiti, lazima awe na vifaa vya utafiti ambavyo vitamwezesha kuipata data aliyokusudia kwa ukamilifu wake.Data ni habari ambazo mtafiti anakusanya.Data lazima iweze kuwa ni ya kutosha kujibu tatizo la mtafiti na iwe yenye urazini.Kifaa kinachotumika kiwe ni kile ambacho kitamsaidia mtafiti kupata data ya kutegemeeka,data ambayo mtafiti ataielewa na kuifasiri vyema bila kupotosha kile kilichokusudiwa na watafitiwa.

Ili utafiti uweze kufanikiwa,mtafitia anafaa kuelewa vifaa ambavyo anaweza akavitimua katitka ukusanyaji wa data, ili ajue manufaa na udhaifu wa kila kifaa na jinsi ambavyo vifaa hivi vinaweza kutumika na  labda kifaa kimoja kikatuka kuridhia mapungufu ya kifaa kingine ili aweze kupata data ya kutegemeeka na kutosheleza utafiti wake.

 

Changamoto zinazomkumba mtafiti katika  utafiti nyanjani

Gharama ya utafiti.

Huenda gharama ya utafiti ikawa kubwa kiasi cha mtafiti  kutoimudu.mtafiti huenda akakosa pesa za kusafiria kwendakatika jamii mbalimbali au kununulia vifaa  mbalimbali vya utafiti ambavyo vinaweza kuwa ni vya bei ghali.Suala la gharama pia huenda likawa kizingiti kwa mtafiti ikiwa atahitajika kusafiri mara nyingi  nyanjani  au kufanya utafiti wake nje ya nchi ambapo labda atahitajika kusafiri kwa ndege.

katika hali ya ukusanyaji  na uhifadhi data,  gharama  ni jambo ambalo lazima lizingatiwe kuna baadhi ya vifaa ambavyo gharama yake huwa ni ghali mno kwa mfano kamera  ambazo zinahitajika katika unasaji wa picha,vifaa vya kuhifadhi data na vinasa sauti.Vile vile wale wataalamu wa vifaa hivi watakaoandamana na mtafiti nyanjani kuvitumia vifaa hivi katika
ukusanyaji wa data huhitaji kulipwa mwishoni mwa shughuli ya ukusanyaji wa habari. Ili kutatua tatizo la gharama mtafiti lazima kwanza  aratibu shughuli zote zitakazohitaji pesa ili aweze  kukadiria kiwango cha pesa ambazo atazihitaji kukamilisha shughuli yake ya utafiti, asije akakwama katika utafiti wake.Pili lazima mtafiti afanye matayarisho ya kutosha kabla ya kujitoza nyanjani kwenda kutafiti kwa kuweka akiba ya kutosha ya fedha ambazo zitamwezesha kuukamilsha utafiti wake.

Vile vile mtafiti anafaa atumia mbinu mwafaka kama vile sampuli ili aweze kupunguza idadi ya elementi katika  jumuiya yake,hali hii itamwezesha mtafiti kufanya  utafiti wake kulingana na uwezo wake wa kifedha.Mwisho mtafiti pia anaweza kutatua tatizo hili kwa kutafuta ufadhili kutoka kwa wahisani na serikali ili kumwezesha kufanya na kuukamilisha utafiti wake.

Matumizimabaya ya pesa zilizotengewa utafiti.

Mtafiti anaweza akatumia pesa zilizotengewa utafiti kwa masuala ya binafsi au kwa mambo ambayo hayahusiani na utafiti uliofadhiliwa.Mtafiti huweza kukabiliwa na changamoto ya kuzitumia pesa ambazo amezitengea utafiti hivi kwamba akawa hana pesa  za kukamilisha utafiti wake. Hali  kama hii ikitokea mtafiti huenda akatoa matokeo  ambayo hayawakilishi jumuiya ambayo alikuwa akiitafiti,au akalazimika kudanganya katika data yake na kutoa matokeo ambayo ni ya kupotosha uma.

Katika kitatua tatizo hili mtafiti anahitajika kuzingatia nidhamu ya utafiti .Mtafiti azingatie nidhamu katika matumizi ya pesa,hususan aweze kuepuka gharama ambazo hazihusiana na utafiti unaofanywa.Vile vile  aweze kuwajibika kwa kutoa kiwango cha wastani katika kila kazi inayotekelezwa ambayo inahitaji malipo,asilipe kiwango cha juu zaidi ambacho labda kitaashiria matumizi mabaya ya pesa au kiwango cha chini zaidi ambacho kinaweza kusababisha ufanyaji wa kazi chapwa.

 Ukosefu wa maarifu ya kutosha katika mbinu za utafiti.

Mtafiti anaweza kukosa maarifa ya kutosha katika kuzitumia mbinu za utafiti.Mtafiti  huenda akawa amesomea zile mbinu lakini haelewi kuzitumia  (to put theory into practice) .Katika utafiti,kuna aina nyingi za mbinu ambazo mtafiti anaweza akazitumia katika ukusanyaji wa data yake ingawa mbinu hizi zote zinategemea ujuzi alionao mtafiti katika kuzitumia.Baadhi ya mbinu zinahitaji ujuzi wa hali ya juu ili kuweza kuzitumia vyema na kupata matokeo yaliyokusudiwa.Baadhi ya mbinu hizi ni kama vile:mahojiano,kujaza hojaji,saveyi,skeju,kesi stadi,mahojiano ya kina na upigaji picha.

Ili kutatua tatizo hili lazima mtafiti awe anaelewa vyema uwanja anaoufanyia utafiti na kisha ajue vyema  aina tofauti tofauti za mbinu za ukusanyaji data ili aweze kutathmini manufaa au uzuri wa kila mbinu na matatizo yake ili awe na uwezo wa kuchuja na kuchagua mbinu ambazo ni faafu zaidi kwa kuzingatia sehemu yake ya utafiti.Vilevile  maarifa katika kutumia mbinu tofauti tofauti za ukusanyaji wa data kutamwezesha mtafiti kuzitumia mbinu hizi kwa pamoja  kuridhia upungufu wa  mbinu zingine  ili kupata data a inayofaa kwa shughuli za utafiti.

Ufasiri wa data

Changamoto nyingine ambayo watafiti ukumbana nayo nyanjani ni ufasiri wa data ambayo wanaikusanya.Kuna baadhi ya mambo ambayo hutokea nyanjani ambayo hupewa  na mtafiti fasiri tofauti na iliyokusudiwa na mtafitiwa.Hali hii husababisha upotoshaji wa matokeo yatakayotolewa na mtafiti.Mfano mzuri wa upotoshaji ni pale ambapo jumuiya ambayo mtafiti anaifanyia utafiti  ina utamaduni na imani tofauti na ile yake au lugha ya watafitiwa  ni tofauti na ile ya mtafiti.Katika hali kama hii kuna baadhi ya mambo ya kitamaduni au imani za watafitiwa ambayo huenda yakafasiriwa vibaya au mtafiti akakosa kuelewa baadhi ya ishara ambazo zinatumiwa na watafitiwa na akazipa maana tofauti akizingatia  tajriba  ya lugha yake  Vile vile tatizo hili linaathiri fasiri ya baadhi ya mambo ya kitamaduni toka lugha asilia ya mtafitiwa hadi lugha ya pili
ya mtafiti.Kuna baadhi ya tamaduni ambazo  ni vigumu kuzieleza kwa lugha ya pili au baadhi ya maneno ambayo yanapatikana katika lugha ya watafitiwa  ambayo hayana visawe vyake katika lugha ya mtafiti.hali kama hii inaweza kuleta upototoshaji wa habari itakayotolewa na mtafiti. Ili kuweza kutatua tatizo hili ni vyema mtafiti kufanya utafiti wake katika jumuiya anayoielewa vyema,kuelewa utamaduni au hata lugha ya watafitiwa ili kuepuka tatizo hili la kufasiri data kwa njia isiyo sahihi. Na ikiwa lazima afanye utafiti katika jamii ambayo haelewi utamaduni wake,lazima afanye uchunguzi wa kutosha ili aweze kufahamu angalau kiasi kidogo cha utamaduni wa jumuiya husika utakaomwezesha kufanya utafiti au aandamane na msaidizi wake ambaye anatoka katika jamii ambayo  anaifanyia utafiti.

Ufinyu wa uelewa juu ya utafiti

Watafitiwa wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya dhana nzima ya utafiti, kwani wengi uamini kuwa mtafiti atapata faidakubwa zaidi kuliko wao pindi atakapo kamilisha utafiti wake.hali kama hii husababisha watafiti kutoshiriki katika utafiti au wakatoa habari za uongo kutokana  na imani potoshi watakayokuwa nayo kuhusiana na utafiti unaofanywa.Pia katika hali hii ya kukosa uelewa juu ya utafiti husababisha watafitiwa labda kuomba kulipwa kwa kutoa habari ambayo inamsaidia mtafiti katika uchunguzi wake,jambo kama hili husababisha gharama ya utafiti  kuwa ghali mno na hata kumfanya mtafiti  asiafiki matakwa yake.

Ili kutatua tatizo hili ni vyema mtafiti kuchukua muda wake na kuwaelezea watafitiwa lengo lake la kufanya utafiti na kisha kuwaeleza kwa kina kama kuna njia wanaweza kinufaika kutokana na utafiti ambao yeye kama mtafiti anatekeleza. Vile vile, mtafiti ahakikishe kuwa halazimishi kupata habari kutoka kwa watafitiwa.Mtafiti  apate data kutoka kwa watu  ambao wanahiari kushiriki katika utafiti wake.

Baadhi ya mbinu za ukusanyaji wa data zinahitaji watu walioelimika

Kuna mbinu  ambazo hutumika katika ukusanyaji wa data  mbazo ni za wale tu walio na uwezo  wa kusoma na kuandika.Mbinu kama hizi huwa na upungufu mkubwa kiasi kwamba wale watakaoshiriki  katika utafiti ni wale tu ambao ni wasomi.Mbinu kama hii huwa na ubaguzi unaoweza kusababisha upatikanaji wa  data ambayo si wakilishi.Kwa mfano, ikiwa mtafiti anafanya utafiti katika sehemu ambayo watu ambao ni wasomi ni wachache,atalazimika kuhoji hii idadi ndogo ya watu na kuitumia kama data wakilishi.

Hivyo basi,data atakayoipata mtafiti haitakua inaiwakilisha vyema jumuiya husika. Katika jumuiya kuna wale watu ambao si wasomi lakina wanaweza kuwa elementi muhimu katika utoaji wa habari ambayo mtafiti anahitaji.Kwa mfano matumizi ya hojaji ni mbinu ambayo ni ya kibaguzi,inawabagua wale wasiojua kusoma kwa kutowashirikisha kutokana na hali yao ya kutojua kusoma na kuandika.Pia katika mbinu hii,kuna wale ambao wana mtazamo hasi wa  kuhusu ujazaji wa hojaji  huenda  ukawafanya wengi  wao kutojaza hojaji hizo. Kutatua tatizo hili,mtafiti anafaa kuelewa vyema jumuiya anayoifanyia utafiti.Aweze kuelewa kiwango chao cha elimu na lugha zinazotumika katika jumuiya husika ili aweze  kuchagua mbinu bora zaidi katika ukusanyaji wa data.mbinu ambayo itakuwa ni jumuishi,itakayozingatia jumuiya nzima bila kubagua kwa misingi yeyote.

Mfumko wa kiuchumi (inflation)

Mtafiti naweza akaadhirika na mfumko wa kiuchumi.Kabla ya kwenda kufanya utafiti nyanjani, mtafiti huandika pendekezo la utafiti.sehemu mojawapo katika pendekezo la utafiti uhusiana na  makadirio ya fedha ambazo mtafiti anatarajia kuzitumia katika utafiti wake.Hali hii huenda ikaadhiriwa na uchumi wa nchi ambao hubadilika kwa kutegemea mambo tofauti tofauti.vile vile dunia nzima  huenda ikawa inapitia hali kama hii ambapo gharama  ya maisha  inapanda kwa jumla.

Ikiwa gharama ya maisha itakuwa inapanda,mtafiti atakuwa na changamoto  hasa kama  atakuwa ashapewa fedha na mfadhili.Utafiti utatatizika kwa sababu bei ya vitu  kama vile vifaa vya utafiti,kodi ,nauli na pesa za kuwalipa wasadizi wa mtafiti itapanda zaidi juu ya makadirio ambayo mtafiti atakuwa amepangia.

Ili kukabiliana na tatizo hili mtafiti anafaa kufanya matayarisho ya kutosha kabla ya kujitoza nyanjani.Aelewe mfumo wa kiuchumi wa nchi ili awe na uwezo wa kubashiri mwelekeo uliopo wa kiuchumi ikiwa unaweza ukawaadhiri katika utafiti wake kabla ya kwenda nyanjani.

Wanajamii wengi kushuku kwamba  mtafiti anawapeleleza  na kukataa kutoa habari.

Katika utafiti kuna uwezekano wa baadhi a wanajamii kuhisi kwamba wanapelelezwa na mtafiti,hali kama hii husababisha watafitiwa kitoshiriki vyema katika utafiti au watafitiwa  kutoa habari za kupotosha ambazo si za kweli kuhusiana na maswali ya mtafiti.wanajamii inafaa wawe tayari kushiri katika utafiti unaofanywa na kuhisi kuwa woa ni muhimu katika utoaji wa habari za
kumsaidia mtafiti kukamilisha malengo yake. Kulingana na Graham Hitchcock (19198) anasema kuwa ,hatua ya kwanza  ya mtafiti akiwa nyanjani ni kuwajibikia  watafitiwa.Anaeleza kuwa mtafiti anafaa ajenga uhusiano wa kirafiki na  watafitiwa. 

Ili mtafiti kukabiliana na tatizo hili,inafaa awaeleze watafitiwa  madhumuni ya utafiti ile kuwafanya waelewe kuwa mtafiti si mpelelezaji bali anakusudia kupata habari kwa shughuli tofauti.vilevile inafaa mtafiti waeleze watafitiwa ikiwa kuna njia watakayonufaika kutokana na utafiti anaoufanya.na vilevile baada ya mtafiti kutekeleza haya yote lazima awahusishe wale tu ambao  wako tayari kushiriki katika utafiti na mwisho mtafiti anafaa akishafanya utafiti  asitumie utafiti huo kwa kuhujumu jamii au jumuiya husika,ahakikishe kuwa anazingatia maadili ya utafiti.

Vizingiti vya kidini.

Hivi hutokea pale ambapo baadhi ya wahojiwa  wanaamini kwamba matendo Fulani yanaenda kinyume na imani yao ya kidini na hivyo kukataa kuhojiwa.utafiti waweza ukaadhirika ikiwa watafitiwa watakosa kushiri katika utafiti.hali hii inaweza kusababishwa na imani ya kidini ambapo watafiti wanakosa kutoa habari ambazo mtafiti anazihitaji.

Ili kutatua tatizo hili mtafiti aelewe imani ya watafitiwa vyema kabla ya kuanza utafiti wake ili aweze kujua jinsi ya kuuliza maswali ambayo labda sio ya moja kwa moja.Anaweza akauliza maswali kwa njia ambayo mtafitiwa atahiari kutoa maoni yake kuhusiana imani ya kidini na kisha ikampa nafasi mtafiti kupata habari za kimsingi kuhusiana na suala analolitafitia.

Hali ya anga.

Vifaaa vya utafiti kama vile vinasa sauti,videorekoda na santuri huweza kuadhirika na hali ya anga kama vile mvua ,kupotea au hata kuharibika  na kupoteza habari zote ambazo zilikuwa zimehifadhiwa.hali ya anga pia hukua changamoto kwa watafiti wengi kwa sababu huadhiri hata usafiri na shughuli nzima ya utekelezaji wa utafiti.Hii inaweza kusababisha utafiti ukachukua muda zaidi ya ilivyotarajiwa na pia vilevile gharama ya utafiti ikaongezeka ili kuweza kukamilisha shughuli nzima ya utafiti. Kukabiliana na changamoto hii, mtafiti anafaa afanye ziara  nyanjani ya matayarisho ya awali kabla ya kwenda kuufanya utafiti wenyewe,hali hii itampa picha ya yale atakayotarajia kukumbana nayo nyanjani na pia kumpa nafasi ya kujitayarisha kukabiliana na hali ya anga tofauti tofauti  nyanjani.

Vikwazo kutoka kwa watawala.

Watawala huenda wakakosa kutoa idhini  ya kufanya  utafiti.mtafiti anaweza kukosa kupata ruhusa ya kufanya utafiti kutokana na vikwazo vya kiutawala.Huenda wakati mwingine akakosa kupata ruhusa ya kufanya utafiti sehemu Fulani kutokana na hofu ya matokeo ambayo uchunguzi huo unaweza kuwa nao kwa watawala.Kwa mfano katika serikali huenda ikawa ni vigumu sana kumruhusu raiya wake ambao ni wataalamu katika Nyanja Fulani kufanya utafiti sehemu kama vile,katika vyuo vya mafunzo ya polisi,ofisi za wakuu wa serikali,ubalozi  na  sekta ya usalama kwa jumla .Serikali  huenda ikahofia matokeo ya utafiti huo katika usalama wa nchi.Vile vile kuna mambo  ambayo yanachukuliwa  na uzito kuwa ni ya kimsingi zaidi katika taifa lolote na yanapaswa tu kuwa siri ya serikali wala si kwa mwananchi yeyote.

Kusuluhisha tatizo hili mtafiti lazima azingatie nidhamu ya utafiti. Afanye utafiti wake  kwa mambo ambayo anajua  hayaendi kinyume na sheria za watawala.Vile vile kabla ya kuuanza utafiti atafute kibali kutoka kwa watawala kitakachompa ruhusa
ya kuendelea na utafiti wake kabla ya kuanza shughuli nzima ya utafiti, ili kusije kukatokea na tatizo mbeleni ambalo litatatiza utafiti.

Matumizi ya data ya watafiti wengine.

Utafiti wowote ule  huhitaji data ambayo itachanganuliwa ili itoe  maelezo ya kueleweka.Kothari anaeleza kuwa baadhi yawatafiti hutumia data ya   watafiti wengine  ambao wamekwisha fanya  utafiti  tofauti na wao.katika kufanya hivi  huenda  data  hiyo isifae  utafiti wake  na hivyo matokeo yakawa  mabovu. Wao   huchukua data  ya watafiti wengine kisha wakairekebisha kusudi iafiki utafiti wao.Matokeo yake baada  ya kuufanyia uchanganuzi utafiti hauonyeshi   ukweli wa suala  linalofanyiwa utafiti.

Kutatua tatizo hili watafiti wanafaa kuzingatia maadili ya utafiti kusudi waweze kutoa repoti ambayo ni wakilishi kwa jumuiya ya utafiti.Hali hii itafanikisha malengo makuu ya utafiti  hivyo basi utekelezaji nao utafanyika kwa njia bora zaidi kwani ripoti hiyo itakuwa ni picha halisi ya jumuiya husika.

Wadhamini mara nyingi ndio huamua mambo yanayochunguzwa

Mara nyingi katika utafiti uliofadhiliwa,wadhamini  ndio uamua mambo yanayochunguzwa,mahali pa kuchunguziwa na mwanda au upeo wa uchunguzi wenyewe.Aidha fasiri ya ufafanuzi wa data mara nyingi lazima  ilingane na masilahi  ya wadhamini.Ikiwa mtafiti atatoa fasiri isiyowiana  an mapendeleo ya wadhamini,huenda mapendekezo yake  yakafutiliwa mbali na pengine  udhamini  wa utafiti zaidi ukasitishwa.Aidha,matokeo ya utafiti mara nyingi huwa mali ya  mdhamini ambaye huweza kuyatumia kuikandamiza jamii ya mtafiti.

Ili kutatua tatizo hili wadhamini wanafaa kumpa mtafiti uhuru wa kufanya utafiti wake bila vikwazo vingi ili aweze
kufanya utafiti amba ni wa ndani na ambao unaweza kutoa mambo mengi ambayo mengine labda hayawezi yakajitokeza ikiwa mtafiti amewekewa vikwazo,lakini mambo hayo yakawa yanahusiana moja kwa moja na  na kila mtafiti anakitafiti.kwa hivyo ni bora mtafiti apewe nafasi yake ili aweze kufanya kazi yake vyema kwa kutumia utaalamu alionao bila ya vikwazo
vya aina yeyote.

Ukosefu wa muda wa kutosha katika utafiti

Mtafiti huenda asiwe na muda wa kutoshakatika ukusanyaji wake wa data au kuwahoji watu wengi.Mtafiti akikosa muda wa kutosha uenda akakosa   habari za kutosha  kuhusiana na mada yake ya utafiti.Hali kama hii hutokea sana hasa kama mtafiti amechukua eneo pana la mipaka ya utafiti ( scope and limitation of research) ,hivi basi hali hii humlazimu mtafiti kufanya utafiti wake katika eneo pana zaidi.Utafiti kama huu huenda ukahitaji muda zaidi wa kutafitia jambo husika.

Sababu  ya pili ya kufanya mtafiti kuchukua muda mrefu katika utafiti wake  ni ikiwa mtafiti ametumia vifaa ambavyo  vinachukua muda  kupata majibu. Kwa mfano,ikiwa mtafiti atatumia  hojaji huenda  ikahitaji muda kujazwa na kisha kutumwa kwa mtafiti, ambapo ni shughuli ambayo inachukua muda zaidi ikilinganishwa na kifaa kama utumiaji wa mahojiana ambayo mtafiti anapata majibu yake ya maswali ya utafiti na kuondoka nayo. Sababu ya tatu ni kuwa, ikiwa mtafiti atafanya utafiti wake kwa kutumia jumuiya pana, hivyo basi itamlazimu pia kuchukua muda mwingi katika jumuiya husika ili aweze kupata data ambayo anahitaji.

Ili kuweza  kutatua tatizo hili,kwanza kabisa lazima mtafiti aweze kubana zaidi mipaka  yake ya utafiti (scope of research) ili aweze kuekeleza utafiti wake kikamilifu kwa muda ambao ameutenga kwa utafiti anaoufanya.hali hii pia itamsaidia mtafiti kupunguza gharama ya utafiti kwa sababu eneo atakalokuwa akishughulikia litakuwa finyu kiasi cha yeye kuweza kuridhia matarajio yake kwa wakati ufaao.

Pili mtafiti anafaa kuibana jumuiya yake ya utafiti  kwa kuiteuwa sampuli ambayo anajua kuwa ana uwezo wa kufanya utafiti kwa muda ambao ameutenga kuufanya utafiti huo.Katika hali hii mtafiti inafaa ateuwe sampuli ambayo anajua kuwa itawakilisha vyema jumuiya na kisha kuioji  na kupata data ambayo anajua kuwa itakuwa ni wakilishi.

Mwisho ni kuwa, mtafiti lazima pia ajue kuwa kuna baadhi ya mbinu ambazo huchukuwa muda mrefu kabla ya kupata data. kwa hivyo, mtafiti achague mbinu faafu zaidi ambazo zitamwezesha kupata data kwa wakati ambao ameutengea utafiti wake.Mtafiti anaweza akatumia kifaa kama vile  skeju ambacho kitamwezesha kuondoka na majibu yake pindi tu amalizapo kumhoji mtafitiwa.

Matatizo ya mawasiliano na uchukuzi

Mtafiti huenda akakumbwa na tatizo la kimawasiliano na watafitiwa hali kama hii hutokea pale ambapo lugha anayoizungumza mtafiti ni tofauti na ile ya watafitiwa.Hii ni kumaanisha kwamba mtafitiwa ana imani na utamaduni ambao ni tofauti  na watafitiwa.Changamoto kama hii huweza kusababisha utoaji wa ripoti ambayo inapotosha. Kwa sababu ikiwa mtafiti haelewi kile ambacho kinazungumziwa basi data atakayoikusanya itakua ni ya kukisia tu wala si  data halisi toka nyanjani.kikwazo cha mawasiliano huwa cha kimsingi sana katika ukusanyaji wa data yeyote kwa sababu katika jumuiya ikiwa mawasiiano yameathirika hivyo basi  utafiti pia utakua umetaizika kwa sababu lugha ndio hubeba mawazo ya binadamu na lugha ndio huwakilisha tabia na utamaduni wa binadamu kwa hivyo  mtafiti ikiwa hatakua na uwezo wa kuwasiliana hivyo basi hataweza kuelewa utamaduni na mambo muhimu katika ukusanyaji wa data yake

Katika uchukuzi,ikiwa mtafiti analazimika kwenda mbali kukusanya habari,hasa katika sehemu kame,itakuwa vigumu kufika huko kwa sababu ya ukosefu wa vyombo vya usafiri kama vile magari. Hali kama hii itasababisha ukosefu wa data,hivyo basi kuathiri utafiti.Ikiwa mtafiti hatakuwa na uwezo wa kuifikia jumuiya hivyo basi hamna utafiti ambao utakua unafanyika,hali hii inaweza kusababishwa na ukosefu wa barabara nzuri,hali ya usalama au hata majanga kama vile mafuriko.

Ili kutatua vikwazo hivi lazima mtafiti aweze kuandamana na msaidizi wake ambaye ana ufahamu wa  utamaduni na lugha ya watafitiwa ile kuwawezesha kupata data wanayoikusudia.vile vile kutatua kikwazo cha uchukuzi mtafiti lazima afanye maandalizi ya awali ili awezi kujua jinsi ya kusafiri kwenda nyanjani anakokwenda kutafuta data.

Matatizo ya kibinafsi kama vile mtafiti anaweza  kushindwa kudhibiti  wale anaolenga kuwahoji.

Matatizo ya kibinafsi.kama vile mtafiti anaweza  kushindwa kudhibiti  wale anaolenga kuwahoji.badala ya yeye kuwauliza maswali,wahojiwa  wanaweza kuwa wao ndio wanaomuuliza mtafiti  maswali.hali kama hii huweza kutokea iwapo mtafiti hana uwezo wa  kujieleza kwa njia ya kushawishi  au  kukosa kuwa na mhalaka  mwema na watafitiwa au mtafiti kukosa kueleza azma yake ya kuufanya utafiti ambao anakusudia kuufanya.  Mtafiti pia anaweza kukumbwa na hali  kama hii  ikiwa ataonesha kutoelewa vyema lengo lake kwa kushuku kiwango chake cha utaalamu  kwa yale ambayo anakusudia kutekeleza.

Tatizo hili linaweza kutatuliwa na mtafiti.anaweza kufanya hivi kwa kufanya matayarisho ya kutosha  kabla ya utafiti kuanza.anaweza akasoma kwa kina kuhusiana na jambo ambalo analitafitia ili awe na uelewa wa mada ya utafiti vile vile aweze kujua maswali atakayouliza na matarajio ya watafitiwa  ili kuweza kuepuka hali ya kutoweza kuuliza maswali yake kwa njia inayoeleweka au kujibu maswali  ya watafitiwa kwa njia inayowaridhisha.

Ukosefu wa usalama

Mtafiti anaweza kuwa katika hali ya kuhatarisha maisha yake wakati anafanya utafiti nyanjani hasa katika sehemu ambazo si salama au sehemu ambazo zimeathirika na vita.ukosefu wa usalama ni changamoto  hasa kwa watafiti wengi ambao huhitajika kufanya utafiti katika sehemu ambazo ni hatari au kufanya utafiti nyakati za usiku.Kwa mfano, mtafiti anaweza kuwa anafanya utafiti wake  kuhusiana na mila na tamaduni  za jamii Fulani ambapo labda  shughuli hizi za kitamaduni hufanyika usiku au akataka kufanya utafiti wake kuhusu sababu za jamii mbili zinazo zozana hapa,mtafiti inabidi ahatarishe maisha yake ndio aweze kupata data.

Kukabiliana na tatizo hili mtafiti nafaa kuomba kupewa usalama kutoka kwa serikali  hasa kama anajua kuwa  sehemu ambayo anafanyia utafiti si salama.Vile vile mtafiti anaweza kuepuka sehemu ambazo ni hatari kwa kuofia usalama wake au afanye utafiti kwa wakati ambao ni salama tu.aepuke kufanya utafiti majira ya usiku.

Matatizo yanayohusina na vifaa

Mtafiti anapokua nyanjani wakati mwingine  vifaa anavyovitumia vinaweza vikakumbwa na  hitilafu na kushindwa kufanya kazi na kumlazimu mtafiti kuacha kazi yake kwa muda  hadi apate kifaa kingine au kilichoharibika kurekebishwa. Vifaa hivi vya utafiti pia huwa na matatizo ya aina mbalimbali katika ukusanyaji wa data.Hakuna kifaa ambacho huwa ni sawa katika matumizi ambacho hakina changamoto.kwa mfano, mtafiti anapotumia kifaa cha kuchukua video huchukua tu sehemu ambayo kinaelekezwa,sehemu ambazo kifaa hiki hakijaelekezwa hakiwezi kunasa picha.Vile vile ikiwa mtafiti anatumia kalamu na karatasi katika ukusanyaji wa data atapata ugumu wa kukabiliana na kasi ya mtafitiwa,vile vile itakuwa vigumu kwa mtafiti kunakili data kama vile ishara za mikono na mwili ,kupanda kwa sauti na kupanda na kushuka kwa sauti.Ili kusuluhisha tatizo hili,mtafiti anafaa kutumia aina nyingi za vifaa vya utafiti ili kuweza kukusanya data kutoka sehemu nyingi za jumuiya.

 

JADILI MANUFAA NA MATATIZO YA VIFAA VIWILI KATIKA VIFUATAVYO:
1.0 Mbinu ya kushuhudia (observation)

Kushuhudia ni mbinu ya kuangalia tukio linapotendeka na kukusanya taarifa zake.

1.1Namna za ushuhudiaji

  1. a) Uchunguzi na upimaji (k.m. katika jiografia, muziki)

Mtafiti awe na vifaa vinavyohitajika kwa kazi hiyo (k.m. rula, mizani, vipima-sauti)

  1. b) Ushuhudiaji funge mno (highly structured observation)

Hufanyika kwa kutumia mandhari yaliyodhibitiwa na kwa kutumia majedwali yaliyosanifiwa

  1. c) Ushuhudiaji funge (structured observation)

Ni aina ya ushuhudiaji ambao hutoa uhuru zaidi ushuhudiaji huu huchanganya majedwali na mahojiano.katika ushuhudiaji wa aina hii mtafiti huwa  si mshiriki, lakini huangalia na kukusanya taarifa waziwazi.Taarifa za ushuhudiaji husaidiana na taarifa za mahojiano na vidadisi

  1. d) Ushuhudiaji lengani (focused observation)

Mtafiti huangalia tukio au tendo katika mazingira yake asilia bila majedwali. Taarifa hupatikana kutokana na kuzoeana na kuwa na mawasiliano ya muda mrefu na watafitiwa.

  1. e) Ushuhudiaji huru/ usiofunge (unstructured observation)

Hufanywa kwa siri na mtafiti bila mtafitiwa kufahamu na bila mpangilio wa wazi.

1.2 Ukusanyaji wa taarifa za ushuhudiaji

huweza kusanywa kwa kujaza majedwali ambayo hujazwa na mtafiti au msaidizi wake au pia huweza kukusanywa kupitia kwa Uandishi wa taarifa.Taarifa huandikwa wakati wa ushuhudiaji usio wa kificho. Taarifa hizo inafaa ziwe na mambo yafuatayo: Tarehe, mahali,wakati, mtu au watu wanaohusika ,vifaa, maelezo ya lengo la shughuli, maelezo ya mandhari,mfuatano wa matukio, ufafanuzi wa shughuli zilizofanyika,hisia na ukereketwa wa wahusika Katika utafiti huu mtafiti anaweza  Kupata
taarifa za nyongeza kutokana na:mazungumzo,mahojiano,nyaraka,rekodi za kanda za video, pichatuli na chati, michoro na ramani

1.3 ufasiri ya taarifa (interpretation of data)

Katika ufasiri ya taarifa za uwanda huu wa kushuhudia inafaa itokane  na kushirikisha watafitiwa wenye ufahamu wa mambo hayo yanayotafitiwa, isitokane na hisia au mawazo ya mtafiti mwenyewe tu

 1.4 Faida na upungufu wa utafiti wa kushuhudia

 Faida

  1. a) Humwezesha mtafiti kukusanya taarifa kwa mpangilio mzuri.katika kushuhudia mtafiti huwa na uwezo wa kuangalia jinsi
    matukio yanavyotokea  kwa utaratibu na hali hii inampa mtafiti nafasi ya kuchukua data kwa kuzingatia utaratibu huo wa
  2. b) Mtafiti huweza  kutaamali matendo na matukio ya kijamii moja kwa moja yanapotokea.wakati mtafiti anashuhudia jambo Fulani likitendeka,yeye huwa na uwezo wa  kulielewa tendo lile
    moja kwa moja kwa misingi kuwa atakuwa anatumia hisi zake zote kupata habari.atakuwa annatumia uwezo wake wa kuona linalotendeka,kusikia kinachoendelea kunusa,kuonja na hata kuguza ili aweze kuwa na uhakika wa habari
  3. c) Pia kifaa hiki humwezesha mtafiti kuchunguza duru za shughuli au tabia katika mazingira yake asilia ya kijamii.Katika hali hii mtafiti huweza kupata data au habari ambazo ni za kuaminika na kutegemeeka kwa sababu mazingira ambamo matukio yametokea ni mazingira halisi.hakuna utiaji wa chuku katika habari unazozitafuta ikilinganishwa na baadhi ya vifaa vingine
    vya utafiti ambapo watafitiwa huenda wakatoa habari ambazo watia chumvi.
  4. d) Humwezesha mtafiti kuchunguza namna watu wanavyoishi na kufanya kazi bila kuingilia shughuli zao.kifaa hiki cha utafiti kina manufaa kwa mtafiti kwa sababu htafiti haadhiri watafitiwa.kwa hivyo habari zinazopatikana kutokana na mbinu hii huwa ni za kuaminika hasa mahali ambapo tafiti hashiriki katika tendo ambalo analifanyia utafiti.hivyo basi huwa ni data ambayo haiegemei wala kuwa na mhemko wa aina yeyote
  5. e) Mtafiti huweza kukusanya taarifa ambazo haziwezi kupatikana kwa njia ya mahojiano au mazungumzo.mtafiti huweza kupata taarifa ambazo mtafitiwa labda hangeweza kuiari kuzitoa kutokana na usiri ambao umo katika utamaduni,kutoruhusiwa na dini au siri za aina yeyote katika jamii.
  6. f)   Utafiti wa kushuhudia huwa ni njia inyomwezesha mtafiti kupata taarifa nyingi kwa gharama ndogo.katika hali ya kushuhudia mtafiti huweza kupata habari kwa kina na kwa gharama ya chini kwa sababu katika mbinu hii hakuna vifaa maalumu vinavyohitajika ila tu ni makini ya mtafiti na uwezo wake wa kutumia macho na  jumla ya hisi zake vizuri(senses).
  7. g) Utafiti kupitia Uchunguzi  unaweza kuchukua mtindo mbalimbali; kwa mfano, mtafiti anaweza kutumia:ushuhudiaji funge
    mno(highly structured observation)- kwa kutumia mandhari yaliyodhibitiwa,ushuhudiaji funge(structured observation)-unaotoa uhuru zaidi kwa mtafiti,ushuhudiaji lengani(focused observation)-ambapo mtafiti huangalia tukio/tendo katika mazingira yake asilia bila majedwali,ushuhudiaji huru (unstructured observation)-ambao hufanywa kwa siri na mtafiti bila mtafitiwa kufahamu na bila mpangilio wa wazi.

upungufu

  1. a) baadhi ya shughuli au matukio yanayochunguzwa hayawezi kufikiwa au kuonekana na mtafiti.katika utumiaji wa kifaa hiki kuna baadhi ya matukio ambayo mtafiti hana uwezo wa kuyafikia  na kuwashughulikia kwa kina kwa mfano mambo ambyo mtafiti anayazingatia ni yale ambayo ni ya kuonekana tu (observable features).mtafiti hana uwezo wa kuelewa hali ya kisaikolojia ya watafitiwa wala  au hata kujua hisia na matamanio yua watafitiwa ambayo hayawezi yakabainika wazi kupitia kwa kushudia tu.
  2. b) wakati mwingine, kuwapo kwa mshuhudiaji huweza kupotosha au kuathiri shughuli inayohusika.katika ushuhudiaji mtafiti anaweza akaathiri shughuli nzima ya utafiti kwa kuwafanya watafitiwa wakafanya mambo labda kwa hali ambayo wanatia chumvi ili kuvutia au wakaona soni na kukosa kufanya baadhi ya mambo katika uasilia wake.
  3. c) njia hii hufaa zaidi kwa matukio ya wakati uliopo; haifai kutumika kuchunguza matukio yaliyopita au ya zamani.mbinu hii inakuwa faafu tu kwa yale matukio ambayo yanatendeka wakati Fulani.Haiwezi kutumika kushughulikia matukio ambayo yashapita.
  4. d) Njia hii haifai kwa kukusanya taarifa kuhusu mikabala, maoni, nia, maana, n.k.njia hii ya ukusanyaji data kutokana na sifa yake kuu ya kutegemea ushuhdiaji wa matukio itakua ni vigumu kwa mtafiti kuelewa hali yakisaikolojia inayompitikia mtafitiwa wala kupata maoni ya mtafitiwa kuhusu jambo ambalo analitafiti
  5. e) njia hii haifai kwa kuchunguza makundi makubwa ya watu.njia hii si bora katiak kufanya utafiti katika makundi makubwa
    ya watu kwa sababu mtafiti hawezi kuwa na uwezo wa ku
  6. f)   huweza kuchukua muda sana, na haifai kwa kuchunguza mwenendo au mchakato kwa muda mrefu sana.mbinu hii huchukua muda mrefu katika kukusanya data na hivi kwamba mtafiti analazimika kukaa nyanjani kwa  muda kabla ya kupata data ya kutosha katika utafiti wake

1.5. Baadhi ya njia za utatuzi wa changamoto hizi

  1. a) katika kutatua tatizo la kuwaadhiri watatitiwa,Kama inawezekana, mtafiti ajifanye mshuhudiaji-mshiriki.mtafiti
    aweze kushiriki katika jambo ambalo analitafiti.
  2. b) mtafiti anafaa kuchunguza kwa kina watafitiwa ili kupata imani ya wale anaowatafiti kwanza (hili huchukua muda).ili kuepukana na tatizo la kwenda kinyume na imani,itikadi,mila na desturi za watafitiwa.
  3. c)  Pia mtafiti anaweza kuufanya uchunguza wake  bila ya kuonekana. Anaweza akaufanya utafiti wa siri akachunguza jumuiya au jamii husika  bila ya wao kujua  ingawa hili nalo lina matatizo yake.
  4. d) Jaribu kuwapo bila kuvutia nadhari ya washiriki.mtafiti pia anaweza akawepo na kuhakikisha kuwa havutii
    makini ya washiriki.mtafiti anaweza kufanya hivyo kwa kujishusha na kujiweka katika kiwango cha  watafitiwa,anaweza
    pia kuvalia kwa njia ambayo inamfanya  aingiliane vyema na watafitiwa.kwa mfano ikiwa mtafiti anafanya uchunguzi katika jamii ya wamaasai anaweza akavaa ngozi jinsi wanajamii hawa wanafanya ili asionekane tofauti na wao.

Uchunguzi yaliyomo (content analysis)

 Ni mbinu ambayo inahusika na uchanganuzi  wa data kutoka kwa  vitabu, majarida  na maandishi mbali mbali.ni mbinu ambayo ni ya kitaalamu ambayo inahusisha kuchambua maandishi yaliyo andikwa na watu tofauti tofauti.Harold Lasswell aneleza kuwa katka uchunguzi yaliyomo jambo la msingi ambalo huchunguzwa ni,nani amesema nini?,anamwambia nani?,kwa nini
anamwambia?,na ni kwa kiwango kipi anaadhirika

Faida za uchanguzi yaliyomo

Ni rahisi kutumika katika ukusanyaji wa data hususan kutokana na urahisi wa kupatikana kwa data kutoka kwa makala mbalimbali yaliyoandikwa.njia hii huwa ni rahisi kutumika kutokana na urahisi wa kupatikana kwa data,data hupatikana  kutoka kwa
makala mbali mbali ambayo yashaandikwa na watu tofauti tofauti.

Gharama yake si ghali kwa sababu  mtafiti hupata data ambayo tayari imekwisha tafutwa toka nyanjani.njia hii huwa  gharama yake si ghali mno kwa sababu ya urahisi wa kupatikana kwa data. Kupitia kwa mbinu  hii mtafiti ana uwezo wa kupata  data kutoka kwa makala ya zamani au miaka  mingi iliyopita.makala ya miaka mingi iliyopita yanaweza yakarejelewa na makala haya yakawa ya manufaa  kwa mtafiti.

Data ambayo hupatikana kupitia mbinu hii huwa haina mhemko kwa sababu mtafiti hana nafasi ya kuathiri data kutokana na yeye kutokuwa na nafasi ya kukutana moja kwa moja na jumuiya anayoitafiti. Data ambayo hupatikana ni data ambayo huwa na urazini (objectivity)

Upungufu

Data zinazopatikana zinaweza kuwa na mapendeleo hivyo basi mbinu hii ikatumika kuendeleza mapendeleo hayo.Ikiwa kosa lilitokea katika ukusanyaji wa data,kosa hili husambazwa kwa mtafiti wa pili ambaye pia husaidia katika kuliendeleza kosa lilo hilo.njia hii basi katika hali kama hii inakosa ya kutegemeeka kwani habari ambazo inazitoa zinaweza kuwa si za kweli.

Data inayopatikana naweza kuwa katika mpangilio ambao huandamani utafiti unaofanywa,hivyo basi kuifanya data hiyo kuwa isiokuwa na manufaa katika utafiti.kuna uwezekano kuwadata ambayo inapatikana  aktika vitabuimepangiliwa kwa njia ambayo haiandamani na utafiti ambao mtafiti anaufanya.kwa mfano mtafiti anaweza kuwa anafanya utafiti kuhusiana na data ambayo anataka habari za kina na vitabu atakavyo kuwa navyo viwe vimepangiliwa kwa majedwa na ramani ambazo labda hazitampa mtafiti habari anazozihitaji.

Data ambayo inapatikana huenda ikawa imepitwa na wakati (obsolete data) hivyo basi kuifanya kuwa isiyokuwa na maana katika utafiti (irrelevant data).Baadhi ya data ambazo hupatikana huenda zikawa zimepitwa na  wakati kutokana na  kasi ya
ubadilikaji wa mambo ya kielimu na teknolojia ya kisasa.

HITIMISHO

Katika karatasi hili Suala ambalo linajitokeza wazi  ni kwamba watafiti  wengi hukumbana na vizingiti na vikwazo vingi katika harakati zao za kutafuta data nyanjani . Jambo ambalo ni la msingi ambalo mtafiti anafaa kujua ni kuwa  vikwazo hivi visimvunje moyo kwani katika jambo lolote ambalo binadamu hujihusisha nalo huwa ni kama sarafu,huwa na pande mbili ambazo ni   uzuri utokanao na utafiti na vile vile changamoto.

Kwa hivyo,mtafiti aweze kutilia maanani umuhimu au faida zitakazotokana na utafitia wake.aweze kupea uzito  mchango atakaoufanya katika Nyanja atakayokuwa ameizamia katika utafiti .Mtafiti asihofu changamoto ambazo anaweza
kumbana nazo nyanjani. Vile vile kutokana na sehemu ya pili,inafaa mtafiti aweze kuelewa aina mbali mbali za vifaa vya utafiti,aelewe jinsi ya kutumia vifaa hivi katika mazingira mbalimbali ili aweze kuwa na uweza wa kujua manufaa na udhaifu wa kila kifaa na jinsi ambavyo vifaa hivi vinaweza kuingiliana nakuridhia upungufu wa vifaa vingine hivyo basi kumpa mtafiti nafasi ya kupata data ambayo ni ya kutegemeeka.

 

 MAREJELEO

Adam, J na
Kamuzora, F (2008) Research Methods for Business and Social Studies.Morogoro: Mzumbe Book Project.

Bowern, C(2008) Linguistic Fieldwork: A Practical Guide. New York: Palgrave- Macmillan.

Kothari, C.R (2004) Research Methodology: Methods and Techniques. New Delhi: New International.

Msokile, M (1993) Misingi ya Uhakiki wa Fasihi. Nairobi: EAEP.

Mulokozi, M.M. (1983) “Utafiti wa Fasihi Simulizi” katika TUKI Makala ya Semina ya Kimataifa ya Waandishi wa
Kiswahili III: Fasihi. Dar es Salaam: TUKI.: kur. 1-25.

        Ogechi, N.O, N.L  Shitemi, na K. I. Simala (wah) (2008) Nadharia katika Taaluma ya Kiswahili na
Lugha za Kiafrika. Eldoret: Moi University Press.

Pons, Valdo (Mh) (1992) Introduction to Social Research. Dar es Salaam: DUP.

         Sewangi, S.S. and Madumulla J.S. (eds) (2007) Makala ya Kongamano la Jubilei ya TUKI (Vol. I and II) Dar es Salaam: TUKI.

Simala, K.I. (mh) (2002) Utafiti wa Kiswahili. Eldoret: Moi University Press.



Leave a Reply

scroll to top