Fasihi ina dhima kubwa katika jamii:
(a) Fasihi ni kitambulisho cha jamii za binadamu. Fasihi hufungamana na miktadha fulani ya kiuchumi, kijiografia na kitamaduni. Kwa hivyo, dhima mojawapo ya fasihi ni kusawiri hali ya binadamu, mazingira anamoishi, mahusiano na mtagusano wake na watu, hisia, imani na mitazamo ya watu katika jamii. Haya huwasilishwa kupitia kwa tanzu na vipera vya fasihi. Methali kama Mke ni nguo mgomba kupalilia inaonyesha imani ya jamii husika ambayo humchukulia mwanamke kama kiumbe anayestahiki kutunzwa na kwamba akivishwa vizuri atakuwa mrembo. Mke anafananishwa na mgomba ambao ukipaliliwa utanawiri na kuzaa ndizi nzuri
(b) Fasihi hueneza itikadi zinazotawala jamii husika. Methali na vitendawili ni mifano ya semi ambazo hutumiwa kutilia nguvu itikadi fulani kwa kuzipitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Fasihi pia inaweza kupinga itikadi zinazotawala, ikachukua msimamo wa kuwatetea wanyonge, Vipera vya fasihi, kama vile nyimbo, hutumiwa kueneza propaganda za kisiasa na kupinga utawala dhalimu. Katika fasihi andishi, maandishi mengi yamepinga ukandamizaji wa wanyonge na kueneza siasa za ukombozi. Baadhi ya kazi za aina hii ni pamoja na tamthilia ya Kinjeketile, ambayo pamoja na kupinga unyonyaji wa mabepari kwa tabaka la wafanyakazi, inawachochea kuungana kupigania uhuru wao wakiongozwa na Kinjeketile mwenyewe.
(c) Fasihi hupumzisha, huburudisha na huliwaza. Nyimbo za kazi husaidia kupunguza hisia za uchovu. Aidha, usomaji wa riwaya, tamthilia na mashairi hupumzisha akili na kuiliwaza. Vivyo hivyo, watu wanapotazama michezo ya kuigiza huchangamka na kujisahaulisha kwa muda matatizo yao.
(d) Fasihi huhifadhi na kurithisha maarifa au elimu ya jamii, Fasihi simulizi na andishi huhifadhi maarifa ya kijamii na kuyapitisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Kupitia kwa tungo, kama vile nyimbo na vitabu (riwaya, ushairi, tamthilia na hadithi fupi), maarifa hupitishwa kwa wanajamii. Amali za jamii (mila, imani, historia) na sherehe za kijadi (jando, matambiko, ibada na sherehe za kutawazwa) huhifadhiwa katika tanzu na vipera vya fasihi simulizi na andishi na kupitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine
(e) Fasihi husaidia kukuza lugha. Lugha ndiyo malighafi ya fasihi. Kila fanani au mwandishi ana upekee wake wa matumizi ya lugha. Kadiri lugha inavyotumiwa na fanani na waandishi mbalimbali, ndivyo nayo inavyofinyangwa upya na kupevuka, na hivyo, matumizi yake kupanuka. Halikadhalika, misimu inapokubalika kama semi katika lugha hukuza lugha kwa kuiongezea msamiati. Maneno yaliyokuwepo katika lugha hupewa maana mpya
(f) Fasihi humwezesha binadamu kujenga tabia ya kudadisi na kutafakari kuhusu masuala yanayomkumba. Katika kusoma kwa makini na hata kuhakiki kazi za kifasihi kama vile riwaya, hadithi fupi na tamthilia, pamoja na tanzu za fasihi simulizi za ngano, semi na vipera vyake, binadamu huimarisha mazoea ya kusoma na kuchunguza makala mbalimbali. Aidha, mtu hupanua mawazo yake na kuweza kutathmini mambo kwa mitazamo mbalimbali.
(g) Fasihi huhamasisha wanajamii kuhusu masuala ibuka na nyeti katika jamii yao. Kwa vile fasihi husawiri mambo yanayoathiri jamii mahususi, msomaji, mtazamaji ama msikilizaji wa kazi ya fasihi hufahamishwa kuhusu mambo mapya au yaliyozuka. Ngomezi, kwa mfano. ilitumiwa kuarifu watu kuhusu tukio jipya kama kuwepo kwa wavamizi, kifo au kualika kwenye sherehe.
(h) Fasihi huadilisha. Fasihi hufunza tabia njema inayokubalika na jamii Huasa jamii dhidi ya matendo hasi na kudumisha maingiliano mema pamoja na hulka zinazokubalika Methali nyingi, kwa mfano, huonya dhidi ya matendo maovu kwa nia ya kukuza maadili.(i) Tamaa mbele mauti nyuma – uonya dhidi ya tamaa. (ii) Mgaagaa na upwa hali wali mkavu – huhimiza bidii. (iii) Ndugu mui heri kuwa naye – huhimiza udugu. Hadithi za kimapokeo pia hutumiwa kufunza maadili. Mathalani, ngano za mhusika fisi huonya dhidi ya tamaa. Ngano za kiayari nazo huonya dhidi ya ulaghai, usaliti, ujinga au utegemezi. Katika novela Kipendacho Roho ya Pauline Kyovi, Nyanya anawahadithia wajukuu wake hadithi ya Kadzo na Mazimwi ili kuwaonya dhidi ya kuhadaiwa kuhusu mapenzi na ndoa. Hadithi hii pia inawaonya dhidi ya kuwaamini watu wasiowafahamu
i) Fasihi huunganisha na kuibua hisia za kizalendo au utaifa. Kupitia kwa nyimbo za kisiasa kama vile wimbo wa taifa, kwa mfano, wanajamii huhamasishwa kuungana pamoja na kuitetea na kuijenga nchi yao. Ufuatao ni mfano wa wimbo unaohimiza uzalendo.
j) Fasihi huhifadhi historia ya jamii. Tanzu kama vile visakale na visasili hueleza historia au asili ya jamii na mambo au vitu vinavyopatikana katika jamii hiyo Tanzu za fasihi andishi pia huhifadhi historia ya jami kimaandishi, Mathalani, tamthilia ya Kinjeketile ni hifadhi ya vita vya Majimaji nchini Tanzania (1905-1907) na hali ilivyokuwa chini ya utawala wa Kijerumani