Ni kipashio kidogo kabisa cha kifonolojia kinachoweza kubadili maana ya neno. Hivyo basi, fonimu ina maana, kwakuwa inaweza kubadili maana ya neno inapobadilishwa nafasi katika neno husika. Foni chache zilizoteuliwa kutoka katika bohari la sauti ili zitumike kwenye mfumo wa sauti za lugha mahsusi ndiyo fonimu. Hivyo, fonimu ni chache ikilinganishwa na foni. Idadi ya fonimu za lugha hutofautiana kati ya lugha moja na nyingine. Mathalani, Kiarabu kina fonimu ishirini na nane (28), Kiswahili kina fonimu thelathini (30), Kifaransa kina fonimu thelathini na tatu (33), na Kiingereza kina fonimu arobaini na nne (44). Sauti ambayo huweza kubadilishwa nafasi yake katika neno lakini maana ikabaki ileile huitwa alofoni.
Alofoni ni kipashio cha kifonolojia kinachotaja hali ambapo fonimu moja hutamkwa na kuandikwa tofautitofauti bila kubadili maana ya neno. Mfano:
Fedha na feza
Sasa na thatha
Heri na kheri
Kwa kifupi, alofoni ni matamshi tofautitofauti ya fonimu (sauti) moja.