FONIMU KAMA ZILIVYO JADILIWA NA MORRIS SWADESH

 Mwanisimu huyu anaifasili fonimu kama kipashio kidogo kabisa kinachoweza kuleta tofauti kati ya maneno yanayofanana ambayo hutambuliwa na msemaji mzawa wa lugha kuwa ni tofauti. Swadesh kama Bloomfield naye anazichukulia fonimu za lugha kuwa vitu ambavyo vinatambuliwa na msemaji mzawa wa lugha. Lengo la Swadesh ni kujaribu kuonesha njia tofautitofauti ambazo tungeweza kuzitumia kugundua fonimu za lugha maalumu. Njia hizo ni kama zifuatazo:

(i)                 Kigezo cha kutobadilika kwa maneno: “Iwapo tutakuta tofauti za matamshi za neno lilelile moja [pasipo tofauti ya maana], basi ichukuliwe kuwa zinaonesha namna kadhaa tu za mkengeuko (unaokubalika) wa vijenzi vya fonimu

(ii)               Kigezo cha mlandano kiasi: Ukilinganisha seti zote za maneno ambayo yanafanana kifonetiki, utafikia mahala ambapo utakuta kuna sauti kadhaa muhimu zinazojitokeza kwa mfano, jozi mlinganuo finyu katika maneno kama vile; dada-data, punga-bunga, koti-goti.

(iii)             Kigezo cha uhusiano usiobadilifu. “Tuchukulie kuwa tuna kipashio cha kifonimu ambacho ni changamani, ambacho moja ya elementi zake au zote hujitokeza katika kipashio kingine changamani bila kuharibu muungano wa uchangamani wake. Katika hali kama hiyo tunaweza kusema sauti zote zenye elementi hiyo huunda darajia moja ya kifonimu.

(iv)             Kigezo cha mgawanyo wa kimtoano: Kigezo hiki kina maana kwamba   “Sauti za fonimu moja hazitaweza kutokea katika mazingira mamoja ya kifonimu. Lakini ili nguvu ya kigezo hiki iweze kufanya kazi, shurti iendane na kigezo cha mlandano wa kifonetiki”

(v)               Kigezo cha mlandano wa ruwaza: “Maumbo fulani maalumu shurti yakubaliane na ruwaza ya jumla ya kifonimu ya lugha inayohusika” Kigezo hiki kinaendana na kigezo (iv). Sauti mbili zinaweza kutokea katika mazingira ya kimtoano lakini kama hazikukaribiana sana kiumbo kiasi cha kuzifanya zionekane kuwa katika darajia asilia moja, kwa mujibu wa ruwaza ya lugha inayohusika, haziwezi kuwa ni sauti za fonimu moja.

(vi)             Kigezo cha jaribio la mbadilishano: Hiki ni kigezo kitumikacho kuonesha kama kubadilisha sauti moja kwa nyingine bado kutaiacha sauti katika mkengeuko unaokubalika.

Kwa ujumla, mambo yanayojitokeza hapa ni kama vile; utaratibu wa kujaribu kuibaini fonimu na fasili ya  tabia ya fonimu.

hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top