FONIMU ZA KISWAHILI

 Kuna mgawanyo bayana wa fonimu za lugha ya  Kiswahili. Kuna makundi mawili yaliyojikita katika kuangalia namna sauti hizo zitolewavyo

Irabu/vokali, nazo zipo 5

Konsonanti, zipo 26

IRABU

Tofauti iliyopo kati ya utamkaji wa irabu na ule wa konsonanti ni kuwa utamkaji wa irabu hauandamani na mzuio wowote wa mkondo-hewa, yaani hewa hupita kwa urahisi bila kuzuiliwa. Hivyo basi, migawanyo ya irabu haitegemei mzuio wa hewa, bali hutegemea sana mkao wa ulimi katika kinywa wakati wa utamkaji, vilevile mkao wa midomo wakati huo. Irabu hupangwa kufuatana na vigezo vitatu: ulimi uko juu kiasi gani kinywani (ujuu); ni sehemu gani ya ulimi inainuliwa au kushushwa (umbele); na midomo ikoje wakati huo (uviringo).

(i)                 UJUU

Wakati wa kutamka irabu-juu ulimi unakuwa umeinuliwa juu katika kinywa, ambapo irabu-chini hutolewa wakati ulimi umeteremshwa chini. Irabu-juu ni kama [i,u] na irabu-chini ni kama [a]. Ulimi ukiwa katikati ya kinywa, irabu zinazotolewa huitwa irabu-kati, nazo ni kama [e,o].

(ii)               UMBELE

Wakati ulimi unainuliwa kinywani, unaweza kupelekwa mbele katika kinywa, na hivyo kutolewa irabu-mbele kama [i,e]. Ikiwa ulimi utarudishwa nyuma, basi irabu zitolewazo zitakuwa irabu- nyuma kama [u,o]. Irabu [a] kama ya Kiswahili hutolewa ambapo ulimi hauko mbele au nyuma, bali uko katikati.

(iii)             UVIRINGO

Wakati wa utamkaji wa irabu, midomo inaweza kuviringwa, na irabu zitakazotolewa zitakuwa  viringo, kama [u,o]. Midomo inaweza kusambazwa au kupanuliwa na hivyo kutoa irabu siviringo, kama [i,e,a].

KIELELEZO CHA IRABU ZA KISWAHILI

[i] irabu juu mbele siviringo

[u] irabu juu nyuma viringo

[e] irabu kati mbele siviringo

[o] irabu kati nyuma viringo

[a] irabu chini siviringo

VIYEYUSHO

Ni aina ya vitamkwa/fonimu  ambavyo si konsonanti na wala si irabu; yaani ni vitamkwa ambavyo huchukuliwa kuwa viko katikati ya irabu na konsonanti. Kwa vile vitamkwa hivi havina sifa kamili ya ukonsonanti na pia havina difa kamili ya uirabu lakini vinaelekea zaidi kufanana na irabu wakati mwingine hupewa jina la nusuirabu. Katika lugha nyingi za Kibantu viyeyusho huwa ni vya aina mbili:

[y] na [w].

KONSONANTI

Konsonanti ni aina ya sauti ambazo hutamkwa kwa kuzuia mkondohewa kutoka mapafuni, ukipitia chemba ya kinywa na chemba ya pua kwenda nje. Uzuiaji wa mkondo huo wa hewa unaweza  kuwa wa kubana kabisa na kuachiwa ghafla, kama tunapotamka sauti [p]; unaweza kuwa wa kubana kabisa na kisha kuachiwa taratibu, kama tunapotamks sauti [ch]; unaweza kuwa wa kubana kiasi na kuruhusu hewa hiyo ipite katika nafasi nyembamba  na wakati huohuo midomo ikiwa katika hali ya kuviringwa  kiasi, kama tunapotamka sauti [f] au [v]; unaweza kuwa wa kubana hewa lakini ukiwa unaruhusu hewa ipite pembeni mwa ulimi, kama tunapotamka sauti [l]; unaweza kuwa wa kubana hewa kinywani na kuiruhusu ipitie puani kama tunavyotamka sauti [m],  [n], an ng’ [ŋ]. Kila konsonanti za lugha huwa na sifa mahsusi zinazozitambulisha.

SIFA KUU ZA KONSONANTI

Sifa hizi zinazingatia mambo makuu matatu

1.      Jinsi konsonanti zinzvyotamkwa

2.      Mahali ambapo konsonanti hutamkiwa

3.      Hali ya nyuzi sauti

SIFA ZA JINSI YA MATAMSHI

Katika sifa hii konsonanti hugawika katika makundi sita

A.    VIPASUO/VIZUIWA

Wakati wa utamkaji wa konsonanti hizi huwa kuna mzuio wa mkondohewa na kuachiwa ghafula. Konsonanti hizi zimepewa jina hilo kutokana na kwamba katioka kuachiwa ghafla kwa mkondohewa sauti itokeayo huwa kidogo kama ina mlio wa kupasua. Kwa mfano konsonanti /p/, /b/, /t/, /d/, /k/ na /g/.

/p/  kipasuo sighuna cha midomo

/b/ kipasuo ghuna cha midomo

/t/ kipasuo sighuna cha ufizi

/d/ kipasuo ghuna chaa ufizi

/k/ kipasuo sighuna cha kaakaa laini

/g/ kipasuo ghuna cha kaakaa laini

B.     VIZUIO/VIPASUO KWAMIZA

Konsonanti hizi zinapotamkwa hewa husukumwa nje kwa nguvu na kuzuiwa halafu nafasi ndogo huachwa ili hewa ipite ikiwa na mkwaruzo. Kwa mfano, /č/ na ŧ/

C.     VIKWAMIZI

Katika utoaji wa sauti hizi mkondohewa unazuiliwa nusu tu, na hivyo hewa           inapita kwa kujisukuma kupitia katika nafasi au uwazi mdogo uliopo, na hivyo          kusababisha kukwamakwama. Kwa mfano, /f/, /v/, /ө/, /ð/, /s/, /z/,  na /š/.

D.    NAZALI

Ni aina ya konsonanti ambazo hutamkwa kwa kukishusha kimio kwa namna ambayo kiasi kikubwa cha hewa kutoka mapafuni huelekezwa kupitia kwenye chemba cha pua. Kwa mfano, /n/, /m/, /ŋ/ n.k.

E.     VITAMBAZA

Hutamkwa kwa hewa kusukumwa nje na kuzuiwa halafu kuruhusiwa kupita pembeni mwa kizuizi bila mkwaruzo mkubwa sana. Kwa mfano, /l/.

F.     VIMADENDE

Hutamkwa ncha ya ulimi ikiwa imeugusa ufizi lakini kutokana na nguvu ya hewa inayopita kati ya ncha ya hiyo na ufizi ncha ya ulimi hupigapiga kwa harakaharaka kwenye ufizi. Kwa mfano, /r/.

SIFA ZA KONSONANTI ZA MAHALI PA MATAMSHI

Sifa hii inahusu sehemu mbalimbali za chemba ya kinywa ambapo alasogezi na altuli hugusana au hukaribiana katika utamkaji  wa sauti tofautitofauti za lugha. Kuna sifa saba za mahali pa matamshi:

SAUTI ZA  MIDOMO

Wakati wa kutamka sauti hizi midomo huwekwa pamoja. Kwa mfano, /p/, /b/ na /m/

SAUTI ZA MDOMO-MENO

Wakati wa kutamka sauti hizi mdomo na meno ya juu hugusana. Kwa mfano, /f/, na /v/.

3. SAUTI ZA MENO

Wakati wa kutamka sauti hizi ncha ya ulimi hugusana na meno ya juu. Mfano wa sauti hizi ni kama vile /ө/,  / ð,

4. SAUTI ZA UFIZI

Sauti hizi zinapotolewa ncha ya ulimi hugusana na ufizi. Mfano wa sauti hizi ni /t/, /d/, /n/, /s/, /z/, /l/, na /r/

5. SAUTI ZA KAAKAA GUMU

Sauti hizi hutolewa wakati sehemu ya nyuma ya ulimi inapogusana na kaakaa gumu. Kwa mfano /č/, /š/, /ј/, n.k.

6. SAUTI ZA KAAKAA LAINI

Sauti hizi hutolewa wakati sehemu ya nyuma ya ulimi inapogusana na kaakaa laini. Kwa mfano /k/, na /g/.

7. SAUTI ZA GLOTA

Sauti hizi hutokea wakatii nyuzi sauti zinapokutanishwa kwa muda mfupi. Katika lugha sauti hizi ni chache sana. Kwa mfano /h/.

HALI YA NYUZI SAUTI.

Katika kongomeo kuna nyuzi-sauti ambazo zinakuwa katika nafasi za aina mbili wakati hewa inapopita. Ikiwa nyuzi-sauti ziko pamoja yaani zimekaribiana au kusogeana karibu hewa inapotoka kwenye mapafu huzisukuma na kuzitenganisha wakati wa kupia, na hivyo kusababisha msukumo. Sauti zinazotolewa wakati huu zinakuwa na mghuno na huitwa sauti ghuna. Ikiwa nyuzi-sauti hizi zimeachana, hewa hupita kwa urahisi bila kuzuiliwa, na hivyo bila kusababisha msukumo. Sauti zinazotolewa wakati huu huwa hazina mghuno, na huitwa sighuna.

hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top