Irabu ni sauti ambazo hutamkwa kwa ulaini bila hewa kuzuiliwa katika ala za sauti.
Irabu za kiswahili ni tano. Nazo ni /a/, /e/, /i /, /o/ , na /u/.kila irabu huwa na sifa zake
Uainishaji wa Irabu
ulimi ndicho kiungo muhimu zaidi katika utamkaji wa irabu/vokali .ulimi huweza kukunjwa kwa njia mbalimbali.
Irabu huanishwa kwa kutegemea vigezo vitatu navyo ni:
- Sehemu ya ulimi inayotumika kutamkia irabu husika (Inaweza ikaw sehemu ya mbele au sehemu ya nyuma ya ulimi)
- Muinuko wa ulimi katika kinywa ( ulimi unaweza ukawa chini, katikati au sehemu ya juu katika kinywa)
- Mkao wa midomo ( midomo inaweza kuwa imeviringwa au kutandazwa)
Kutokana na vigezo hivi irabi hizi tano za kimsingi huwa na sifa zifuatazo ambazo zinatokana na umbo lifuatalo:
Sifa za irabu
- /a/ ni Irabu ya katikati na chini kinywani na midomo ikiwa imetandazwa.
- /e/ ni ya mbele na kati kinywani na midomo ikiwa imetandazwa.
- /i/ ni irabu ya mbele na juu kinywani na midomo ikiwa imetandazwa.
- /o/ ni irabu ya nyuma na kati kinywani na midomo ikiwa imeviringa.
- /u/ ni irabu ya nyuma na juu kinywani na midomo ikiwa imeviringa.
Tazama Jedwali Lifuatalo:
Irabu | Sehemu ya Ulimi ya Kutamkia | Mwinuko wa Ulimi | Mkao wa midomo |
/a/ | katikati | chini | tandazwa |
/e/ | mbele | kati | tandazwa |
/i/ | mbele | juu | tandazwa |
/o/ | nyuma | kati | viringwa |
/u/ | nyuma | juu | viringwa |
Zoezi
- Taja makundi mawili ya sauti za Kiswahili.
- Yatofautishe makundi ya sauti za Kiswahili uliyotaja katika (a)
- Toa mifano miwili miwili ya irabu ambazo hutamkwa:
- midomo ikiwa imeviringa
- midomo ikiwa imetandazwa
- Eleza jinsi irabu /e/ inavyotamkwa.
- Taja aina mbili za ala za kutamkia na utoe mfano mfano mmoja mmoja.