Istilahi zinazotumika katika ushairi

Istilahi za kishairi nimisamiati bainifu  unaotumika kurejelea masuala ya ushairi. Istilahi hizi
ni kama zifuatazo:

Mshororo (mishororo)

  Ni mstari au sentensi moja katika ubeti. Mistari hii inapowekwa pamoja hujumlisha ubeti. Ni kigezo hiki ambacho hutumika kuainisha aina za mashairi. Ubetu ufatao una mishororo Mitano.

 Titi la mama litamu,hata likiwa la mbwa,

Kiswahili naazimu,sifayo iliyofumbwa,

Kwa wasiokufahamu,niimbe ilivyo kubwa,

Toka kama mlizamu, funika palipozibwa,

Titile mama litamu,Jingine halishi hamu.

(Shaban Robert)

Mwanzo 

Ni mshororo wa kwanza katika ubeti. Pia huitwa fatahi ama kifungua.

Mloto

Ni mshororo wa pili katika ubeti.

Mleo

 Ni mshororo wa tatu katika ubeti.

Mshata (mishata)

Ni mshororo katika ubeti wa shairi ambao haujakamilika haswa kimaana na hutegemea mwingine unaofuata ili kupasha ujumbe. Idadi ya mizani pia huweza kuwa si kamilifu ikilinganishwa na mishororo mingine.

Sifa za mishata

1.    Huweza kuishia kwa alama za mdokezo.

2.    Huwa fupi

3.    Huwa na mizani michache ikilinganishwa na mishororo mingine

4.     Haikamiliki kimaana yaani haitoi ujumbe kamili.

5.    Humhitaji msomaji kuwaza jinsi ya kuukamilisha.

6.    Humlazimu msomaji kusoma mshororo mwingine ili kupata ujumbe.

Mistari kifu/toshelezi

Ni mishororo inayojitosheleza kimaana bila kutegemea mishororo mingine. Vilevile idadi ya mizani huwa kamili katika mishororo yote.

Kibwagizo/kiitikio/mkarara/kipokeo 

Aghalabu huwa ni mshororo wa mwisho katika ubeti ambao umerudiwarudiwa katika beti zote.

Mfano ufuatao unaonyeesha mwanzo, mloto, mleo na kibwagizo.

Lugha yangu ya utoto,hata sasa nimekua, ( mwanzo)

Tangu ulimi  mzito,sasa kusema najua, ( Mloto)

Ni sawa na manukato,moyoni mwangu na pua, (Mleo)

Titile mama litamu,jingine halishi hamu. ( kibwagizo)

(Shaban Robert)

Umuhimu wa kibwagizo

1.     Huwa ni kiini cha shairi
yaani hubeba maudhui.

2.     Kupitia kwa kibwagizo
tunaweza kupata kichwa cha shairi iwapo hakikutajwa.

3.  Husisitiza ujumbe wa
shairi.

4.    Huonyesha mwisho wa
ubeti.

Kiishio/kimalizio

Mshororo wa mwisho katika ubeti. Mshororo wenyewe huwa ni tofauti katika beti zote.

Ubeti (beti) 

Ni jumla ya mishororo iliyowekwa pamoja na ambayo hujitosheleza kimaana na hubeba hoja ama ujumbe na
hubainishwa na kuwepo ama kutokuwepo kwa kanuni kuu za utunzi wa tungo.

Mizani  

Ni idadi ya silabi au sauti zinazotamkika katika kila mshororo wa ubeti. 

Mashairi mengi ya arudhi aghalabu huwa na mizani 16 ingawaje huwa siyo lazima. Rejelea mifano inayofuata inayoonyesha mizani katika mshororo.

Hahunalo la kusema, ilasasa kukuaga

ha

tu

na

lo

la

ku

se

ma

i

la

sa

sa

ku

ku

a

ga

1

2

3

4

5

7

7

8

9

10

11

12

13

14

15

16

Vina Ni silabi zamwisho wa kila kipande cha mshororo.

Huainishwa kama vina vya ndani/kati ama vina vya nje/mwisho.Vina huweza kufanana ama kutofautiana. Iwapo shairi lina vipande ziadi yaviwili, vina huainishwa kutegemea vipande kwa mfano vina vya ukwapi,
vina vya utao, vina vya mwandamizi na vina vya ukingo

  Umuhimu wa vina

Vina huwa ni muhimu kwa
sababu zifuatazo:

1.     Huleta mdundo,”rhythm”  na hata burudani kwa msomaji.

2.     Hutambulisha na kupambanua utanzu wa ushairi kwani vina hutumika tu katika mashairi.

Kipande (vipande)

 Ni kijisehemu katika mshororo. Mshororo huweza kuwa na kipande kimoja, vipande viwili, vitatu
au hata vinne.

Ukwapi

 Ni kipande cha kwanza katika mshororo.

Utao 

Ni kipande cha pili katika mshororo.

Mwandamizi

Ni kipande cha tatu katika mshororo.

Ukingo

Ni kipande cha nne cha mshororo.

Utoshelezo 

Ni ile hali ya mtunzi kuandika ujumbe ambao unaeleweka kinagaubaga na ambao unaweza kujisimamia kivyake katika kila ubeti wa shairi. Yaani kila ubeti hutoa taarifa yake kikamilifu pasi na kutegemea ubeti mwingine kukamilisha ujumbe uliokusudiwa.

Arudhi 

 Ni sheria au kanuni zinazotawala utunzi wa mashairi. Suala hili la arudhi haswa hujitokeza sana katika mashairi ya jadi. Kanuni hizi ni kama vile: urari wa vina, mpangilio maalum wa beti, mishororo sawa katika kila ubeti, mizani inayojitosheleza katika kila mshororo, vipande sawa katika kila mshororo n.k.

Muwala

 Ni kule kutiririka kwa mawazo au ujumbe na hata fani kutoka hatua moja hadi nyingine katika
shairi. Ujumbe hufululiza vyema kwa njia ya kueleweka kutoka ubeti mmoja hadi mwingine.

Bahari

Ni mikondo tofauti tofauti ya mashairi kutegemea jinsi shairi lenyewe lilivyoundwa. Bahari za
mashairi zimejadiliwa kwa kina katika sura tofauti.

Diwani

 Hurejelea mashairi mengi yaliyokusanywa katika kitabu kimoja.

Malenga

Ni neno ambalo hutumiwa kuashiria mtunzi wa mashairi.

Manju– ni mwimbaji wamashairi.

 

 

USHAIRI

1.        

Historia ya Ushairi

2.        

Changamoto za ufundishaji na usomaji wa uhairi

3.        

Istilahi zinazotumika katika ushairi

4.        

Sifa za mashairi ya kimapokeo

5.        

Sifa za mashairi huru

6.        

Kategoria kuu za mashairi

7.        

Bahari za mashairi

8.        

Uchambuzi wa mashairi

9.        

Uhuru wakishairi

 

 

hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top