Mashairi huweza kugawika katika
kategoria mbili kuu:
1) Mashairi ya jadi
2) Mashairi huru
Mashairi ya jadi.
Mashairi haya pia huitwa mashairi ya kimapokeo au ya kiarudhi. Aina hii ya
mashairi hufuata kaida za utunzi wa mashairi. Kanuni hizi ni kama vile:
• urari wa vina
• mpangilio maalum wa beti
• mishororo sawa katika kila ubeti
• mizani inayojitosheleza katika
kila mshororo
• vipande sawa katika kila mshororo n.k.
Malenga wanaoshikilia msimamo huu huitwa wanamapokeo. Mashairi yasiyofuata sheria hizi hujulikana
kama guni. Mfano wa shairi la kiarudhi ni kama lifuatalo.
Naja sasa ni ndiyani, naja kwetu Mzalendo
Naja nirudi nyumbani, nilowekwa nako kando
Kwetu’ mi nakutamani, kulo na mwingi uhondo
Nijaye ni yule nyundo, misumari hadharini
Naja kwingine kuwapi, kulojaa langu pendo?
Huenda nende kwinginepi, sawa nako kwa muundo?
Kaa kwingine anapi, ela kwenye lakwe gando?
Nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
Naja nije rudi papo, panigedeme mgando
Ningaambwa kwetu hapo, kwamba kwanuka uvundo
Sitakwenda penginepo, tarudi kuko kwa mwando
Nijaye ni ile nyundo, misumari hadharini
(Limenukuliwa)
Tunaainisha shairi hili kama la jadi kwa sababu:
• Lina urari wa vina; ubeti wa 1 vina ni………‘ni’………….‘ndo’
ubeti wa 2
……………………‘pi’…………….‘ndo
ubeti wa 3
……………………‘po’……………‘ndo’
• Lina mishororo sawa (minne) katika kila ubeti
• Mizani inajitosheleza katika kila mshororo (mizani 16)
• Vipande ni sawa (viwili, yaani ukwapi na utao) katika kila mshororo
• Lina beti tatu zinazojitosheleza.
Mashairi huru
Ni kategoria ya mashairi yasiyozingatia kanuni za utunzi. Hii ina maana ya kwamba kanuni zilizoorodheshwa chini ya mashairi ya kimapokeo siyo lazima zifuatwe. Aghalabu mashairi haya huzingatia maudhui kwa kina. Kila malenga huwa na mtindo wake tofauti wa kuwasilisha kazi yake. Wanaoshikilia msimamo huu nao huitwa wanamapinduzi. Mashairihaya pia huitwa mapingiti/mavue/masivina/zuhali/za kimapinduzi. Hebu tazama shairi lifuatalo.
Nimeyaandika maneno haya kwa niaba ya,
Mamilioni wasio malazi
Wazungukao barabarani bila mavazi
Wabebao vifurushi vilivyo wazi,
… milki yao ya maisha.
Kwa niaba ya:
Maelfu wanaovuma bila haki
Wiki baada ya wiki
Leo sumu au spaki
Leo kamba au bunduki
Na kwa wale wanasubiri kunyongwa
Kwa niaba ya
Vijana walio mtaani
Wale mayatima na maskini
Wazungukao mapipani
Kila pembe mjini
Kuokota sumu kutia tumboni
Kujua bila kujua
’ili kupata kuishi.
Kwa niaba ya:
Wakongwe wasiojiweza
Walao chakula kilichooza
Wachukuao choo wakijipakaza
Pole pole wakijiangamiza
Katika vyumba vyao
Baridi na giza
Kwa saba hawan watazama
Wala wauguza
Mbona tukasema kuwa shairi hilo ni huru?
Ni kwa sababu;
• Halina urari wa vina
• Mizani si sawa katika mishororo yake
• Idadi ya mishororo katika beti ni tofauti
Sifa za mashairi huru
• Huwa hayazingatii idadi sawa ya mishororo katika beti.
• Aghalabu huwa hayana urari wa vina.
• Hayana idadi maalum ya vipande katika mishororo.
• Huwa hayana idadi sawa ya mizani katika mishororo.
• Nyingi yazo huwa na kipande kimoja tu.
• Hutumia mistari mishata.
• Hayana kibwagizo bali huwa na kituo.
• Hutumia takriri kwa wingi.
USHAIRI
2. Changamoto za ufundishaji na usomaji wa uhairi
3. Istilahi zinazotumika katika ushairi
4. Sifa za mashairi ya kimapokeo