Fasihi ina majukumu manne ya kimsingi:
(a) Kuchora au kusawiri mazingira ya binadamu. Fasihi ni kitambulisho cha jamii. Hii ina maana kuwa fasihi huchota maudhui au mambo ya kuzungumziwa kutoka kwa jamii inayohusika. Kupitia kwa fasihi, itikadi na mielekeo ya jamii hueleweka.
(b) Kukuza au kujenga tabia. Katika kuisoma, kuitazama au kuisikiliza kazi ya kifasihi, binadamu hujenga tabia yake. Mathalani, kupitia kwa tungo kama vile hadithi, binadamu huweza kuiga matendo ya wahusika na kujifunza kwayo
(c) Kumburudisha na kumstarehesha binadamu. Msomaji, mtazamaji au msikilizaji wa kazi ya kifasihi hujituliza na kusisimka kimwili na kiakili anapoisoma, kuitazama ama kuisikiliza kazi ya kifasihi. Vilevile, fasihi humpumzisha binadamu na kumtuliza baada ya shughuli za kazi
(d) Kuichochea na kuielimisha jamii. Fasihi hueneza mawazo na falsafa za jamii kwa wanajamii. Huuchochea na kuufumbua macho umma ili kupiga vita mazingira ya njaa, maradhi, umaskini, ujinga na hali nyingine za uozo katika jamii. Pia huwapa wanajamii maarifa na stadi za kukabiliana na mazingira ambamo wanaishi