Zipo njia mbalimbali ambazo hutumika katika kutafsiri, baadhi ya njia hizo ni kama vile:
(i) Tafsiri ya neno kwa neno. [Word to word translation]
(ii) Tafsiri sisisi.[ Literal translation]
(iii) Tafsiri ya kimaana/uwazi.[ Semantic translation]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano.[Communicative translation]
(i) Tafsiri ya neno kwa neno [Word to word translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo mofimu na maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana zake za msingi bila kujali muktadha. Katika aina hii ya tafsiri mpangilio wa mofimu na maneno wa lugha chanzi hubakia vilevile bila kubadilika. Na kwa kawaida matini inayotafsiriwa huandikwa chini ya matini ya lugha chanzi. Tazama mifano ifuatayo ya tafsiri ya neno kwa neno:
Kiswahili: Alisoma hadi asubuhi
Kingereza: He/past/study/until/morning
Kiswahili: Alikimbia mpaka ofisini kwake
Kingereza: He/past/run/until/office/his
Kiswahili: Anasoma kitabu changu
Kingereza: He/present/book/my
Kiswahili: Walikula chakula chote
Kingereza: They/past/eat/food/all
Umuhimu wa njia hii, humsaidia mtu kuelewa muundo wa lugha chanzi na jinsi lugha chanzi inavyofanya kazi, kaina hii ya tafsiri hutumiwa na wataalamu wa lugha kuonesha namna maumbo au muundo wa lugha chanzi ulivyo, lakini mapungufu yake ni kuwa, aina hii ya tafsiri huwa haitoi maana inayokusudiwa kwa uwazi zaidi.
(ii) Tafsiri sisisi [ Literal translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo maneno hufasiriwa yakiwa pweke pweke kwa kuzingatia maana za msingi katika lugha chanzi bila kujali sana muktadha lakini ni tafsiri inayofuata mfumo wa kisarufi hasa kipengele cha kisintaksia ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: He was taken at the Central Police Station
Kiswahili: Alipelekwa kwenye kituo cha kati cha police.
Badala ya kuwa: Alipelekwa kituo kikuu cha polisi
(iii) Tafsiri ya kisemantiki/maana au uwazi [Semantic Translation]
Hii ni aina ya tafsiri ambayo mfasiri huegemea zaidi kwenye lugha chanzi. Katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hufasiri kila neno katika sentensi jinsi lilivyo lakini kwa kufuata sarufi hususani vipengele vya kisemantiki na kisintaksia ya lugha chanzi. Inaitwa tafsiri ya kisemantiki kwa sababu, mfasiri anapofasiri hutakiwa kuweka mkazo kwenye maana ya matini kama ilivyokusudiwa na mwandishi wa matini chanzi.
Katika aina hii ya tafsiri, masahihisho au urekebishaji wa neno au jambo lolote unalodhani limekosewa haliruhusiwi isipokuwa unaweza kuweka hayo marekebisho au ufafanuzi katika tanbihi. Sasa tuangalie baadhi ya mifano ya aina hii ya tafsiri:
Kiswahili: Alikwenda mpaka hospitali
Kingereza: He went up to hospital
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: Jane alimwoa John
Aina hii ya tafsiri, ina faida kubwa katika ukuaji wa lugha lengwa kwa kuingiza miundo ya misemo kutoka lugha chanzi, mathalani, lugha ya Kiswahili imepokea miundo mipya ya misemo kutoka lugha ya Kingereza, baadhi ya miundo hiyo ni kama vile:
Kiswahili: Usiku mwema ? kutoka Kingereza: Good night
Kiswhili: Mabibi na mabwana ? kutoka Kingereza: ladies and gentlemen
Kiswahili: Wako mtiifu ? Kutoka Kiingereza: Yours Sincerel
Kiswahili: Naomba nichukue nafasi hii.. ? Kutoka Kiingereza: May I take this opportunity…
[Tazama pia Mwansoko na wenzake: 2006]
(iv) Tafsiri ya kimawasiliano/ huru [Communicative Translation]
Hii ni aina ya tafsiri inayomlenga msomaji [hadhira] wa matini lengwa, ambaye katika aina hii ya tafsiri hatarajii kukutana na ugumu wowote katika matini atakayoisoma, bali hutarajia kukutana na tafsiri nyepesi ya dhana za kigeni katika utamaduni na lugha yake kwa kadiri itakavyoonekana. Hivyo basi, mfasiri wa aina hii ya tafsiri yuko huru kutafuta maneno na mafungu ya maneno yanayolingana na maneno, methali, nahau, utamaduni na mazingira ya lugha lengwa, pamoja na kuwa tafsiri ya kimawasiliano kufuata sarufi ya lugha lengwa ni lazima pia ifuate utamaduni, mazingira na historia ya jamii ya lugha lengwa. Tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: Jane married John
Kiswahili: John alimwoa Jane
Kingereza: No need to cry over spilt milk
Kiswahili: Maji yakimwagika hayazoleki
Kiingereza: What comes around goes arround
Kiswahili: Mla vya watu, naye vyake huliwa.
Kiswahili: Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli
Kiingereza: A friend in need is a friend in need
Kiswahili: Bahati haiji mara mbili
Kiingereza: Golden chance never comes twice
Aina hii ya tafsiri hulenga kutoa athari ile ile au inayokaribiana kwa hadhira ya matini lengwa kama ilivyo kwa hadhira ya matini chanzi[ matini asilia], hii ni aina ya tafsiri ambayo hutumika sana kufasiri mawazo ya kigeni katika lugha na mazingira mapya, mawazo ambayo huelezwa katika misingi ya lugha, utamaduni na mazingira yanayoeleweka kwa hadhira ya matini lengwa.
Ebu tuangalie baadhi ya mifano tuliyoiangalia katika tafsiri ya Kisemantiki [maana] tunavyoweza kutafsiri katika njia ya tafsiri ya kimawasiliano:
Kiingereza Kiswahili
Good night Lala salama
Ladies and Gentlemen Ndugu zangu
Yours Sincerely Ni mimi
May I take this opportunity to… Naomba mnisikilize
Hivyo basi, katika aina hii ya tafsiri, mfasiri hutafuta methali au misemo inayopatikana katika lugha lengwa inayohusiana au kukaribiana na ile ya lugha chanzi. Ebu jaribu kutafsiri misemo/methali zifuatayo ya lugha ya Kiswahili kwenda lugha ya Kiingereza:
Adhabu ya kaburi aijuaye maiti
Asiyekubali kushindwa si mshindani
Asiyefunzwa na mamaye hufunzwa
Chema chajiuza kibaya chajitembeza
Dua la kuku halimpati mwewe
Bandubandu humaliza gogo
Jogoo wa shamba hawiki mjini
La kuvunda halina ubani
Mtegemea cha nduguye hufa masikini
Faida ya aina hii ya tafsiri, humfanya mfasiri kuwa huru kutumia maneno au mafungu ya maneno ambayo huweza kutoa athari ile ile au inayokaribiana na maneno au mafungu ya maneno katika matini ya lugha chanzi, lakini mapungufu ya aina hii ya tafsiri huweza kutokea iwapo mfasiri ataamua kuegemea mno kwenye mawazo, historia, mazingira au itikadi ya lugha lengwa. Ebu tuangalie mifano ifuatayo:
Kingereza: The Merchant of Venice
Kiswahili: Mabepari wa Venisi
Ukiangalia mfano huo utaona kuwa, The Merchant of Venice, tamthiliya iliyoandikwa na William Shakespeare, ingefaa pia kufasiriwa kuwa, Wafanyabiashara wa Venisi, lakini Mwalimu J.K Nyerere aliamua kuifasiri kuwa, Mabepari wa Venisi kutokana na kuwa Nyerere ndiye mwasisi wa itikadi ya Ujamaa nchini Tanzania, hivyo aliegemea katika itikadi kufasiri.
Hivyo basi, mtu anapokuwa anafanya kazi ya kufasiri, maandishi yo yote kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine atajikuta akiangukia katika moja wapo ya njia tulizozijadili hapo juu, lakini ikumbukwe tafsiri ya neno kwa neno ni nadra sana kutumiwa na wafasiri wengi, na njia hizo huweza kuingiliana katika matini moja ya tafsiri.
Ukalimani [Interpritation]
MAREJEO
Cartford [1995] A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press
Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.
Oxford University Press Dar-es-salaam
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.
D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2018
www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2018
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2018
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman