MBINU ZA UTAMBUZI WA FONIMU

 Ili kuweza kuzibaini fonimu na alofoni za lugha fulani, wanaisimu hutumia mbinu mbalimbali. Miongoni mwa mbinu hizo ni hizi zifuatazo:

(i)                 Mfanano wa Kifonetiki

(ii)               Jozi mlinganuo/ pambanuzi finyu

(iii)              Mgawanyo wa kiutoano

(iv)              Mpishano huru

(I)                MFANANO WA KIFONETIKI

Sauti zinazofanana kifonetiki ni sauti zilizo na sifa bainifu zinazofanana. Kwa mfano irabu zina sifa bainifu zao na konsonanti zina sifa bainifu zao. Sauti zinazofanana sana kifonetiki ni sauti za fonimu moja (alofoni). Kwa mfano, [i] na [u] haziwezi kuwa alofoni za onimu moja kwa sababu sauti hizi zinatofautiana mno kifonetiki. Mfano katika maneno yafuatayo:

(i)                 /Baibui/ na /buibui/

(ii)               /angalau/ na /angalao/

(iii)              /badili/ na /badala/

(iv)              /Akhsante/ na /ahsante/

(v)                /mahali/ na /mahala/

Ni wazi kwamba sauti /u/ na /a/; /u/ na /o/; /i/ na /a/ na /X/ na /h/ kama tulivyosema hapo awali, haziwezi kuwa alofoni za fonimu moja kwani zina tofautiana sana kifonetiki. Labda tunaweza kusema kuwa sauti hizi ni za lahaja tofauti tofauti au zatokana na vyanzo mbalimbali kama ilivyo kwa /X/ na /h/ kwamba /X/ ni sauti ya Kiarabu wakati /h/ ni sauti ya Kibantu. Ukizichunguza irabu /u/ na /a/ kwa mfano, utagundua kuwa mfanano pekee ni kwamba ni irabu lakini hazina mfanano mwingine. Wakati /u/ ni irabu ya juu nyuma viringo, /a/ ni ya irabu ya chini/. Pia /X/ ni konsonanti ya kaakaa laini wakati /h/ ni ya glota. Mfanano pekee unaoonekana ni kwamba zote ni konsonanti na zote ni sighuna.

Daniel Jones (1957) anaeleza kuwa fonimu fulani katika lugha huwa ni ujumuisho na udhahanishaji wa sauti kadhaa au kundi la sauti ambazo kwanza kabisa ni lazima zifanane sana kifonetiki. Anasema ni familia ya sauti (family of sounds); wanafamilia huwa na mfanano fulani kama sura, urefu n.k. Hapa Jones anazungumza kuhusu alofoni

(II)                JOZI MLINGANUO FINYU/ JOZI PAMBANUZI FINYU (minimal pairs)

Fischer (1957) anaeleza kuwa, jozi mlinganuo finyu ni tofauti ndogo kabisa ya kifonolojia iliyopo baina ya maneno fulani.  Mara nyingi maneno hayo huwa na

(i)                 Idadi sawa ya fonimu

(ii)                Fonimu zinazofanana isipokuwa moja

(iii)             Mpangilio wa fonimu ulio sawa

Kwa mfano, katika lugha ya Kiswahili maneno kama /pia/; /tia/ na /lia/ ni jozi mlinganuo finyu kwa sababu zina idadi sawa za fonimu (fonimu tatu), aina za fonimu zilizopo ni sawa isipokuwa moja, yaani /i/ na /a/ ni sawa na tofauti ni /p/, /t/ na /l/. Kigezo hiki ni cha uamilifu. Maneno hayo yote lazima yawe ya lugha inayohusika na pia neno hilo liwe na maana tofauti na neno la awali. Hivyo, sauti /p/, /t/ na /l/ ni fonimu tofauti kwa sababu zinabadili maana ya maneno.

(III)          MGAWANYO WA KIMTOANO/ MTAWANYO MKAMILISHANO (Complementary distribution)

Hyman (1975), anasema, utoano ni dhana ambayo hutumiwa kuelezea uhusiano uliopo baina ya sauti mbili au zaidi za fonimu moja ambazo haziwezi kutokea katika mazingira sawa! Kwa hiyo, kila sauti huwa ina mahala/ mazingira yake maalum ambayo hayawezi kukaliwa na sauti nyingine. Kwa mfano, kutoka katika lugha ya Kiingereza sauti /p/ na /ph/ hutokea katika mazingira tofauti. Wakati /p/ hutokea mahali popote pale, /ph/ hutokea mwanzoni mwa maneno tu kama katika maneno /pin/, /pen/, /put. n.k. Kwa sababu sauti hizo zinafanana kifonetiki na tofauti pekee ni mpumuo tu basi sauti hizo ni alofoni za fonimu moja ambayo ni [p]. Na sauti hizo zipo katika mahusiano ya mgawanyo wa kimtoano.

Katika lugha za Kibantu pia hili hutokea kama inavyojidhihirisha katika data ifuatayo kutoka katika lugha ya Kiruuri.

Mofimu za maneno                       matamshi yake                        maana yake

(xii)           Βirikir+a                            [βirikira]                                  ita

(xiii)         n+βirikir+a                        [mbirikira]                               unite

(xiv)         a+ka+βusi                          [akaβusi]                                  mbuzi mdogo

(xv)           i+n+βusi                            [imbusi]                                   mbuzi

(xvi)         o+gu+βusi                         [oguβusi]                                 buzi kubwa

(xvii)       o+ru+rimi                          [orurimi]                                  ulimi

(xviii)     ji+n+rimi                           [jindimi]                                  ndimi

(xix)         reer+a                                [reera]                                      refu

(xx)            n+reer+a                           [ndeera]                                   ndefu

(xxi)         O+ku+lim+a                      [okulima]                                 kulima

(xxii)       i+n+lim+I                          [indima]                                   namna ya kulima

Utagundua kwamba sauti /b/ na /β/ zinafanana sana kwani zote ni konsonanti za midomo na zote ni ghuna; pia sauti /l/, /r/ na /d/ zote  ni za ulimi; au /s/ na /z/ katika /dogs/ na /cats/ ni sauti za ufizi na tofauti pekee ni +/- ghuna.

[b]/ N——-

/β/      

 [β]/———

Hii maana yake ni kwamba fonimu /β/ inajitokeza kama [b] inapotanguliwa na nazali na inajitokeza kama [β] mahali penginepo.

(IV)          MPISHANO HURU

Ni uhusiano wa fonimu mbili tofauti kubadilishana nafasi moja katika jozi maalumu ya maneno bila kubadili maana ya maneno hayo. Kwa hiyo, maneno mawili yanaweza kuwa na tofauti ya fonimu moja tu lakini fonimu hizo tofauti ni tofauti sana kifonetiki na hivyo haziwezi kuwa alofoni za fonimu moja.

Pili, fonimu hizo hazipo katika ule uhusiano wa kiutoano, yaani, zote zinaweza kutumika katika mazingira yaleyale kwenye neno lakini fonimu hizo ingawa ni tofauti hazisababishi tofauti za kimaana katika maneno zinamotokea. Kigezo hiki hakipingani na kile cha msingi kuhusu uwezo wa fonimu kuweza kubadili maana. Tofauti kati ya mpishano huru na mgawanyo wa kiutoano ni kwamba:

► Mpishano huru huhusisha fonimu mbili au zaidi zilizo tofauti kabisa, mgawanyo wa kiutoano hazihusishi alofoni mbili au zaidi za fonimu moja zinazofanana sana kifonetiki, za aina moja na zinazotamkiwa sehemu moja.

► Mpishano huru huhusisha fonimu mbili zinazobadilishana/kupishana nafasi moja katika neno wakati mgawanyo wa kiutoano huzihusisha alofoni ambazo zimegawana mahali tofauti pa kutokea. Kila moja ina muktadha wake maalumu ambao ni mwiko kukaliwa na alofoni nyingine.

► Kufanana kwao ni: mpishano huru maana za maneno hazibadiliki na pia katika mgawanyo wa kiutoano maana za maneno hazibadiliki.

Baadhi ya mifano ya mpishano huru katika lugha ya Kiswahili:

MANENO

MPISHANO HURU

Alimradi- ilimradi

/u/ na /i/

Baibui- buibui

/a/ na /u/

Bawabu -bawaba

/u/ na /a/

Angalao- angalau

/o/ na /u/

Amkia- amkua

/i/ na /u/

Banyani- baniani

/ny/ na /n/

Wasia – wosia

/a/ na /o/

Heri- kheri

/h/ na /X/

Mtelemko- mteremko

/l/ na /r/

Sababu zinazosababisha mpishano huru:

► Tofauti za kimtindo

► Tofauti za kilahaja

► Tofauti za kijiografia

hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top