MCHAKATO WA KUTAFSIRI/KUFASIRI

 

Mambo ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri.

Hatua muhimu katika kutafsiri Tunapofanya tafsiri kuna hatua muhimu kuu sita kwa mujibu wa Mwansoko na wenzake (2006). Hatua hizo ni kama ifuatavyo:

Maandalizi ya kutafsiri

Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kufahamu vizuri maudhui ya matini chanzi, ujumbe wake, mtindo wa matini na kuwekea alama sehemu zenye utata au zisizoeleweka vizuri, anashauriwa kupigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri au kuyatolea ufafanuzi zaidi katika tafsiri yake.

Uchambuzi wa matini chanzi

Katika hatua hii, mfasiri anatakiwa kuchunguza kwa makini maneno, methali, nahau, misemo pamoja na maelezo mengine ya matini chanzi aliyoyaandika au kuyapigia mstari katika hatua ya maandalizi na kuyatafutia visawe vyake katika lugha lengwa, hapa mfasiri anashauriwa kutumia marejeo mbalimbali kama vile, kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya.

Mfasiri anatakiwa kuwa na shajara au daftari dogo kwa ajili ya kuandika na kuhifadhi maneno na maelezo muhimu ya matini chanzi na visawe vyake, visawe vinavyoonekana kufaa viorodheshwe vizuri ili iwe rahisi kuvirejelea wakati wa kutafsiri, vilevile mfasiri kama ataona kuwa matini chanzi ni ndefu sana, anashauriwa kuigawa matini hiyo katika sehemu ndogondogo kama vile, sura, aya au sentensi na kuanza kushughulikia sehemu moja baada ya nyingine.

Uhawilishaji

Uhawilishaji ni uhamishaji wa mawazo kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa, au uhamishaji wa mawazo au ujumbe kutoka matini asilia kwenda matini ya tafsiri. Hii ina maana kuwa katika hatua hii, visawe vya kisemantiki [kimaana] vya matini chanzi vilivyobainishwa katika hatua ya uchambuzi huamishwa katika matini lengwa [kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa] na kupangwa vizuri kisarufi na kimantiki ili fasiri hiyo iwe na maana kwa wasomaji wake. Katika hatua hii mfasiri uhawilisha ile taarifa kutoka kwenye matini chanzi kwenda kwenye matini lengwa, hapa mfasiri anatakiwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa na lugha chanzi. mfano; “My new car is broken”-langu jipya gari ni vunjika. Tafsiri ya Kiswahili sanifu inapaswa kuwa “Gari langu jipya limeharibika” Uhawilishaji maana yake ni kuhamisha maana, ujumbe nk. kutoka lugha chanzi kwenda lugha lengwa kwa kuzingatia sarufi ya lugha lengwa, lengo la matini au mwandishi, umbo la matini, mtindo nk. Mbinu ya tafsiri ambayo inatumika katika hatua hii ya uhawilishaji ni tafsiri ya neno

 Kusawidi /Kuandaa rasimu ya kwanza ya tafsiri.

Katika hatua hii, mfasiri huandika rasimu yake ya kwanza ili kupata picha fulani ya matini aliyoikusudia, katika uandaaji wa rasimu ya kwanza, kwa kufanya hivi, mfasiri anaweza kugundua kuwa anahitaji taarifa zaidi tofauti na alizozipata katika hatua ya uchambuzi, na hivyo kulazimika kuchunguza zaidi matini chanzi na hata kupekua zaidi na zaidi marejeo yake aliyoyaandaa kwa kuyatumia katika tafsiri. Jambo la kuzingatia, mfasiri anatakiwa wakati akihamisha mawazo au ujumbe azingatie umbo na lengo la matini chanzi ili kutoathiri tafsiri yake. Rasimu ya kwanza ya tafsiri inakuwa na dosari nyingi na kwa hiyo haifai kupelekwa kwa mteja au hadhira. Badala yake rasimu ya kwanza lazima ipitiwe tena upya na kurekebishwa au kudurusiwa/durusu (review) rasimu (draft).

Kudurusu / kuipitia rasimu ya kwanza

Baada ya kusawidi rasimu ya kwanza, mfasiri anatakiwa kuivundika rasimu yake ya tafsiri kati ya juma moja hadi mawili baada ya kukamilika kwake na kuanza kuidurusu/ kuipitia rasimu hiyo kwa jicho la kihakiki zaidi na kuangalia kama kuna makosa ambayo yamejitokeza katika rasimu yake au la na kuyafanyia marekebisho pale inapobidi.

 Kusomwa kwa rasimu ya tafsiri na mtu/watu wengine

Baada ya mfasiri kuipitia rasimu yake ya kwanza, na kuifanyia masahihisho kwa makosa yaliyojitokeza, anatakiwa kuwapa watu wengine waidurusu rasimu hiyo iliyofanyiwa marekebisho ili waipitie tena na kuirekebisha, hivyo basi wasomaji hao wanaweza wakahakiki,wakashauri, n.k. Wasomaji hawa husaidia kuona kama tafsiri iko sahihi, inaeleweka na ina mtiririko mzuri wenye mantiki.

 Usawidi /Kuandika rasimu ya mwisho

Baada ya kupata maoni kutoka kwa wasomaji wa pili, mfasiri anaweza kuyatumia maoni, mapendekezo na maelekezo yao kusahihisha tena tafsiri yake na hatimaye kuandaa na kutoa rasimu ya mwisho ambayo itakuwa tayari kwa kusomwa na wasomaji.


MAREJEO

Cartford [1995] A linguistic Theory Translation

Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na

Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam

Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press

Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.

Oxford University Press Dar-es-salaam

Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.

D.S.M

TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam

TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2018

www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2018

www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2018

Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo

Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla

Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.

William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere

Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere

Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa

Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton

Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman


hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top