NADHARIA YA TAFSIRI

 Nadharia ya tafsiri ndio nguzo au mhimili muhimu wa shughuli zote za tafsiri. Vipengele vingine vitakavyojadiliwa katika nadharia ya tafsiri ni pamoja na taaluma zinazohusiana na tafsiri na dhima ya nadharia ya tafsiri. Sababu za kuanzishwa kwa nadharia za tafsiri. Newmark (1982), Mwansoko na wenzake (2006) wanasema kuna mambo matatu yaliyosababisha kuanzishwa kwa nadharia ya tafsiri ambayo ni:-

i)                    Wingi wa makosa katika tafsiri zilizochapishwa awali; ilionekana kwamba, kulikuwa na makosa mbalimbali kama vile makosa ya kimuundo, kimaumbo, kimsamiati nk. Pia ilikuwa ni nadra/muhali kupata tafsiri zisizokuwa na makosa.

ii)                   Kuwepo kwa idadi kubwa (na inayoongezeka) ya asasi zinazojishughulisha na kazi za tafsiri. Hali hii ilisababisha kubuniwa kwa nadharia ya tafsiri ili kuwepo kwa misingi inayokubalika. Mfano; nchini Tanzania peke yake kuna asasi nyingi zinazojishughulisha na tafsiri kama vile: BAKITA, TATAKI, SHIHATA, WAFASIRI na vyombo mbalimbali vya habari kwa mfano: TV, Magazeti nk.

iii)                 Mfumuko wa istilahi katika taaluma mbalimbali hasa Sayansi na Teknolojia. Hivyo nadharia ya tafsiri ilianzishwa kwa lengo la kuleta ulinganifu wa istilahi hizo kati ya lugha moja na nyingine ili kuwe na ufanisi zaidi.

Kimsingi nadharia za tafsiri zinanuia kutekeleza majukumu yafuatayo:

1.       Kubaini na kufasili (define) tatizo la kifasiri yaani kazi au mlolongo wa shughuli za tafsiri zinazopaswa kufanywa katika utatuzi wa tatizo la tafsiri lililobainishwa.

2.        Kuonesha vipengele vyote vinavyopaswa kuzingatiwa katika utatuzi wa tatizo la tafsiri lililobainishwa.

3.       Kuorodhesha taratibu au njia zote zinazowezekana kufanikisha tafsiri inayohusika.

4.       Kupendekeza taratibu zinazofaa zaidi katika kutekeleza zoezi la kufasiri pamoja na mbinu za kutafsiri zilizomuafaka zaidi kwa matini inayohusika.

A)    Nadharia ya Usawe wa Kimuundo

; nadharia hii inatetewa na mtaalam Catford (1969),kulingana na Catford, tunapofanya kazi ya kutafsiri tunatakiwa kuzingatia ulinganifu wa kimuundo kati ya matini chanzi na matini lengwa, maana yake ni kwamba muundo wa matini chanzi ujitokeze katika matini lengwa. katika nadharia hii muundo ni muhimu. Pia nadharia hii hutumika zaidi katika kutafsiri maandiko ya kidini hasa Biblia.

B.Nadharia ya Usawe wa Kidhima

  Watetezi wa nadharia hii ni pamoja na Nida (1964) na Nida na Taber (1969) wanaona kuwa usawe wa kidhima ni muhimu zaidi kuliko usawe wa kimuundo. Wafasiri wanapaswa kuhakikisha kwamba dhima ya matini chanzi pamoja na athari zake zinajitokeza katika matini lengwa. Yaani kama matini chanzi inawalenga watoto inapaswa iandikwe kiasi kwamba watoto wataweza kuelewa. Pia kwa kuzingatia nadharia hii unapaswa kutumia lugha rahisi na inayoeleweka na watu wote. Vilevile tafsiri yako iwe nzuri kiasi kwamba mtu atakaposoma asiweze kujua kwamba hii kazi imetafsiriwa. C. Nadharia ya Usawe wa Aina-matini

Nadharia hii inaeleza kuwa matini yoyote ile ifasiriwe kwa kuzingatia aina yake. Hii ina maana kwamba kazi itakayotokea ifafanana na matini chanzi. Kama matini chanzi ni ya kisheria itakapotafsiriwa matini lengwa nayo itaonekana kuwa ya kisheria. Katika nadharia hii kinachozingatiwa ni fani  na maudhui  la matini yenyewe inayotafsiriwa. Watetezi wa nadharia hii ni Reiss (1971), Buhler (1965) na Newmark (1982/88)

D. Nadharia Changamani (Cross Fertilization theory).

  Hii ni nadharia tete iliyoasisiwa na P.S.Malangwa (2010) Nadharia hii inadai kwamba huwezi kufanya tafsiri kwa kutumia nadharia moja tu, kwa sababu hakuna nadharia inayojitosheleza yenyewe. Kwa hivyo mfasiri anafaa kujumuisha nadharia zote katka tafsiri ili aweze kuwa na matini lengwa yenye maana iliyokusudiwa na mwandishi wa matin chanzi.



MAREJEO

Cartford [1995] A linguistic Theory Translation

Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na

Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam

Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press

Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.

Oxford University Press Dar-es-salaam

Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.

D.S.M

TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam

TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.

www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2018

www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2018

www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2018

Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo

Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla

Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.

William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere

Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere

Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa

Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton

Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman


hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top