Sifa katika isimu ni vitu au mambo ambayo yanakibainisha kipengele chochote cha kisarufi au cha kiisimu (Massamba 2004:80).
Sifa bainifu ni nduni zitumikazo kutofautisha kipashio kimoja cha isimu na kipashio kingine cha aina yake. Katika kubainisha vipashio mbalimbali kuna vigezo viwili:
A. KIGEZO CHA KIFONETIKI
Kigezo hiki huangalia jinsi, mahali, hali ya nyuzi sauti, mwinuko wa ulimi na umbo la midomo katika utamkaji wa sauti mbalimbali za lugha tofauti tofauti.
B. KIGEZO CHA KIFONOLOJIA
Hiki ni kile kinachoangalia maathiriano ya lugha. Fonolojia nyambulishi ya lugha mahsusi. Hapa sifa za lugha inayochambuliwa huangaliwa zaidi. Kwa mfano, kuna baadhi ya fonimu hupata sifa ya usilabi katika lugha mojawapo na siyo nyingineyo. Mfano, mtu, /m/ inapata sifa ya usilabi. Pia katika nne, /n/ hupata sifa ya usilabi. Aidha, hali hii inalingana na mfumo wa lugha husika.
Wanafonolojia wengi wanakubaliana kwamba wazo la sifa pambanuzi lilianzishwa na shule ya “Mawazo ya Prague”. Hata hivyo mwanazuoni wa kwanza kulibabadua suala la sifa pambanuzi alikuwa ni NIKOLAJ TRUBETZKOY, naye ni mmojawapo kati ya waanzilishi wa Shule ya Mawazo ya Prague. Mwanazuoni huyu alianzisha nadharia ya Upambanuzi (Trubetzkoy 1969:31-83). Madai ya msingi katika nadharia hii ya Trubetzkoy ni kwamba pakiwapo na upambanuzi basi lazima patakuwapo ‘ukinzani’. Naye anauainisha ukinzani pambanuzi katika seti kuu tatu.
SETI YA KWANZA
(a) Ukinzani uwili
(b) Ukinzani kiwingi
(c) Ukinzani kiwiani na
(d) Ukinzani kipeke
(a) UKINZANI KIUWILI (Bilateral Opposition)
Ni ukinzani wa sauti ambapo jumla ya sifa bainifu zinazochangiwa na sauti mbili kinzani hupatikana katika sauti hizo mbili peke yake na si kwingineko. Mfano, vipasuo vya midomo [p] na [b] katika Kiswahili ambavyo vinachangia sifa ya kuwa vipasuo vya kinywa vya midomo, hakuna vipasuo vingine vinachongia sifa hiyo.
(b) UKINZANI KIWINGI (Multilateral Opposition)
Huu ni ukinzani wa sauti ambapo jumla ya sifa bainifu zinazochangiwa na sauti hizo kupatikana katika seti ya sauti nyingine pia. Mfano P na R (herufi) zote zinachangia mkunjo upinde unaoelekea kulia. Lakini haziwezi kuhesabiwa kuwa na ukinzani kiuwili, kwa sababu sizo herufi pekee zenye mkunjo kama huo herufi B nayo inao. Hivyo, ukinzani unaopatikana katika sauti ambazo jumla ya sifa zinazochangiwa nazo hupatikana pia katika ukinzani mwingine na ndio ujulikanao kama ukinzani kiwingi
(c) UKINZANI KIWIANI (Proportional opposition)
Ni ukinzani wa sauti mbili ambao unawiana na ukinzani wa sauti mbili ambao unawiana na ukinzani wa sauti nyingine mbili. Mfano, ukinzani baina ya [f] na [v] na ukinzani baina ya [s] na [z] katika Kiswahili.
(d) UKINZANI KIPEKE (Isolated opposition)
Ni ukinzani ambao ni wa kipekee kabisa. Mfano, ukinzani baina ya sauti [r] na [l] katika lugha ya Kiingereza. Katika lugha hii hakuna memba wengine walio na uhusiano wa namna hiyo.
SETI YA PILI
(a) Ukinzani kibinafsi
(b) Ukinzani kimwachano taratibu
(c) Ukinzani kisawa
(a) UKINZANI KIBINAFSI (Private opposition)
Huu ni ule ukinzani ambapo sauti moja inakuwa na alama za ziada (sifa ya ziada) na sauti nyingine inakuwa haina, mfano kama sauti moja inakuwa na mghuno nyingine inakuwa haina n.k.
(b) UKINZANI KIMWACHANO TARATIBU (Gradual opposition)
Ni ule ukinzani ambapo memba wa seti wanapishana kwa viwango tofauti vya sifa ileile. Mfano, tofauti iliyopo baina ya irabu [o] na [u].
(c) UKINZANI KISAWA (Equipollent opposition)
Ukinzani ambapo ukinzani baina ya memba wa kundi moja ni sawa na ukinzani baina ya memba wa kundi jingine, kimantiki; kwa maana ya kwamba ukinzani wao si wa kupishana kwa viwango vya sifa ileile wala hawawezi kuchukuliwa kwamba kama memba mmoja wa kundi ana sifa ya ziada basi mwingine hana. Kwa mfano, sauti [p] na [t] na [f] na [k] katika Kijerumani.
SETI YA TATU
(A) Ukinzani imara (ukinzani usobadilifu)
(B) Ukinzani usoimara (ukinzani ulobadilifu)
Trubetzkoy pia anaziainisha sifa pambanuzi kwa kuangalia kiasi cha ubainifu wa upambanuzi wa sifa. Mfano, ukinzani baina ya /t, d, l/ katika Kiswahili. /t/ siku zote inakuwa /t/ lakini /l/ inaweza kugeuka na kuwa /d/ mfano, katika u-limi—— n-dimi. Hivyo ukinzani wa /t/ ni imara lakini ule wa /d,l/ si imara (badilifu).