Kuainisha matini ni kuzigawa au kuziweka matini katika makundi mbalimbali kwa kuzingatia kufanana kwake. Tunaainisha matini kwa sababu kila matini inahitaji mbinu maalum ya kuitafsiri.
vigezo vya uainishaji:
Wataalam wengi wanatumia vigezo vitatu ambavyo ni:
v Kigezo cha Mada (Topic/Field)
v Kigezo cha Matumizi ya Istilahi na
v Kigezo cha Dhima kuu za Lugha
1. Kigezo cha Mada
katika kigezo hiki tunaangazia maudhui ya jumla ya matini. Tunajiuliza matini hii inahusu uwanja gani hasa katika maisha? Kwa kutumia kigezo hiki cha mada tunapata aina tatu za matini ambazo ni:
i) Matini za Kifasihi (Literary Text); hizi ni matini ambazo zinahusu fani mbalimbali za fasihi kama vile riwaya, tamthilia, ushairi nk.
ii) Matini za Kiasasi (Institutional Texts); matini hizi ni mtini za kimamlaka kama vile matini za kisiasa na kiserikali (hotuba, risala, mikataba, vyeti nk).
iii) Matini za Kisayansi (Scientific Texts); matini hizi hujumuisha masuala yote ya Sayansi na Teknolojia. Kwa mfano; Fizikia, Kemia, Biolojia nk.
2. Kigezo cha matumizi ya Istilahi:
katika kigezo hiki kinachozingatiwa hapa ni kwamba, matini huainishwa kwa kuangalia wingi au idadi za istilahi-msamiati wa uwanja maalum/husika mf: sharia nk. Kwa kutumia kigezo hiki tunapata aina tatu za matini:
a) Matini za kiufundi (Technical Text), matini hizi huwa na idadi kubwa ya istilahi.
b) Matini za kinusu ufundi (Semi-Techinical Text), matini hizi huwa na idadi ndogo au chache za istilahi.
c) Matini za zisizo za kiufundi (Non Techinical Text), matini hizi ni zile ambazo hazina kabisa istilahi bali hutumia maneno ya kawaida kabisa.
3. Kigezo cha Dhima Kuu za Lugha (Major Language Functions).
Buhler (1965) alipendekeza dhima kuu tatu za lugha ambazo ni:
i) Dhima elezi (Expressive Function), katika dhima hii lugha hutumika kuelezea hisia za mwandishi/mzungumzaji. Anasema, mzungumzaji au mwandishi hueleza hisia zake bila kumjali msikilizaji au msomaji.
ii) Dhima Arifu (Informative Function), dhima hii ya lugha hujitokeza pale ambapo matini au lugha inatumika katika kutoa taarifa kuhusu jambo fulani. Dhima hii huegemea kwenye ukweli wa mambo.
iii) Dhima amili (Persuasive Function) katika dhima hii lugha hutumika kuchochea hisia za msikilizaji au msomaji. Kiini cha dhima hii ni hadhira.
Kwa hiyo, kwa kuzingatia dhima hizi tatu tunapata aina kuu tatu za matini kama ifuatavyo: Matini Elezi (Expressive Texts); matini hizi huegemea upande wa mwandishi. Mwandishi hutumia matini hizi kuelezea hisia zake. Mfano, kazi mbalimbali za kifasihi, hotuba, matini mbalimbali za kimamlaka, matini za kisheria, matini mbalimbali za kitaaluma, maandishi binafsi nk. Pili, Matini Arifu (informative Texts); matini hizi ni zile ambazo zinatoa taarifa au maarifa kuhusu jambo fulani. Sifa yake ni kuwa zinakuwa na umbo sanifu au umbo maalum mfano; umbo la jarida, kitabu, ripoti, tasnifu, vitabu vya taaluma mbalimbali nk. Na mwisho, Matini Amili (Persuasive Texts); matini hizi huegemea upande wa hadhira. Katika matini Amili mwandishi hujitahidi kadiri awezavyo kuchochea hisia za wasomaji na kuwafanya watende kama ambavyo mwandishi anataka watende. Hivyo huegemea upande wa msomaji. Mfano wa matini hizo ni kama vile mialiko mbalimbali, matangazo, maelekezo mbalimbali nk.
MAREJEO
Cartford [1995] A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press
Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.
Oxford University Press Dar-es-salaam
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.
D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2018
www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2018
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2018
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman