Katika sehemu hii tutaangalia mambo muhimu yanayotakiwa kuzingatiwa katika tafsiri, hivyo basi, tutagawa mambo hayo ya kuzingatia katika sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kutafsiri na sehemu ya pili, tutaangalia mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa mchakato wa kutafsiri. Tukianza na:
[a] Mambo ya kuzingatia kabla ya kuanza mchakato wa kutafsiri.
Kwanza unatakiwa kusoma matini nzima.
Mtu anayetaka kutafsiri matini yoyote ile jambo la msingi la kuzingatia ni kuisoma matini nzima tena kwa umakini ili kuelewa maudhui ya matini chanzi, kuweka alama sehemu za matini zenye utata au zisizoeleweka vizuri, hii itamsaidia kubaini ni aina gani ya marejeo muhimu yatakayomsaidia kutafsiri mfano wa marejeo hayo ni kama kamusi, ensiklopedia, orodha ya msamiati na istilahi mpya. Kusoma kwa matini kunamwezesha mfasiri kubaini sifa na vipengele vinavyojenga matini husika kimuundo, kidhima na kiitikadi.
Unatakiwa kubaini lengo la matini chanzi
Malengo ya mwandishi huweza kuwa kukweza, kusifu, kukashfu au kuarifu jambo. Kwa kawaida waandishi wa matini chanzi wanakuwa na mitazamo mitatu; i) Mtazamo hasi kwa mtendwa (biased) mfano, katika gazeti; “Chelsea yaichabanga Arsenal tatu nunge” ii)Mtazamo chanya kwa mtendwa (biased) mfano katika gazeti; “Chelsea yafuta uteja kwa Arsenal” iii) Mtazamo wa kati (neutral) mfano katika gazeti; “Chelsea yaifunga Arsenal au Arsenal yafungwa na Chelsea”
Mfasiri baada ya kusoma matini chanzi anafaa ajiulize ikiwa ameweza kubaini lengo la matini chanzi , Kubaini lengo la matini kunakusaidia kuweza kutafsiri bila kutofautiana au kukinzana na lengo la matini chanzi, mathalani, matini mbili tofauti zinaweza kueleza jambo lilelile na kutumia data zilezile lakini mtindo wa lugha uliotumika unaweza ukaonesha mitazamo miwili tofauti.
Hebu angalia tamthilia ya Mercant of Venice, iliyoandikwa na William Shakespeare na kutafsiriwa na Mwalimu J.K. Nyerere kwa lugha ya Kiswahili na kuitwa Mabepari wa Venisi, kumbuka kuwa tamthiliya hiyo ingeweza kuitwa pia Wafanyabiashara wa Venisi lakini ukiangalia tafsiri ya kwanza [Ya Mwalimu Nyerere] inatupa hisia hasi wakati ya pili huwezi kupata hisia yoyote.{Mwansoko na wenzake 2006:15}
Kubaini lengo la mfasiri.
Mfasiri anapaswa kujiuliza kwa nini nafasiri kazi hii? Je lengo langu na mimi ni tofauti na la mwandishi? – Aepuke upendeleo kwa hadhira chanzi na hadhira lengwa badala yake ajikite katika ukweli. Hivyo inafaa awe katika mtazamo wa kati(neutral) – Kama kuna haja ya kuegemea upande mmoja basi aegemee kwa hadhira lengwa.
Kubaini ubora na mamlaka ya matini chanzi.
Hapa mfasiri hana budi kuzingatia ujuzi wa mwandishi katika kutumia zana za kiisimu/vipengele mbalimbali vya lugha. Mamlaka hutokana na hadhi au ubobevu wa mwandishi huyo katika taaluma au fani aliyoandikia. Mfano, kazi ya fasihi ya S. Robert ni bora kuliko iliyoandikwa na mimi kwa sababu yeye ni mbobevu/galacha katika taaluma hiyo
Unatakiwa kubaini hadhira/ wasomaji lengwa.
Kabla ya mfasiri hajabaini wasomaji au hadhira ya wasomaji wa matini yake ya tafsiri ni vema kwanza akaibaini hadhira ya matini chanzi na ndipo abaini hadhira/ wasomaji mahususi wa matini yake ya tafsiri, maswali anayotakiwa kujiuliza mfasiri ili aweze kuibaini hadhira ya matini yake ya tafsiri ni: je msomaji wa tafsiri yake ni nani? Ana kiwango gani cha elimu, ni msomi wa kawaida au msomi aliyebobea? Wana umri gani na ni jinsia gani? Je hadhira yake imo katika tabaka gani katika jamii? Baada ya kupata majibu ya maswali hayo, mfasiri atakuwa ameibaini hadhira yake,na hii itamsaidia mfasiri kuamua umbo la matini yake, kama ataamua iwe katika umbo la gazeti, jarida, kijarida, n.k. jambo la kuzingatia umbo la matini ya tafsiri ishabihiane na hadhi ya umbo la matini chanzi. Kwa kuibaini hadhira ya matini lengwa itamsaidia mfasiri kuamua kuirahisisha tafsiri yake au kuifanya iwe ngumu kutegemeana na uwezo wa hadhira ya tafsiri lengwa.
Unatakiwa kubaini mtindo wa matini chanzi.
Vilevile, mfasiri anatakiwa kujua, matini chanzi imetumia mtindo gani katika kuwasilisha maudhui yake, imetumia mtindo wa kirasimu? Au imetumia mtindo wa kitaaluma? Je imetumia mtindo wa kiuandishi wa habari au mtindo wa kimawasiliano yasiyo rasmi? Je ametumia lugha rasmi au ya mtaani? Na inatakiwa mtindo wa matini chanzi ilingane na ile ya matini lengwa. Tazama mifano ifuatayo:
Kingereza: Please, Sir do no mind it! If I arrive earlier I’ll wait for you
Kiswahili: Mkubwa! Kausha tu! Na kama nitatia maguu mapema,
nitakusikilizia Palepale
Ukiangalia mfano huo, utaona kuwa, mitindo iliyotumika katika sentensi hizo ni mitindo miwili tofauti, katika mfano tuliouangalia katika lugha chanzi, mtindo wa lugha uliotumika ni mtindo rasmi, wakati katika tafsiri [lugha lengwa] mtindo uliotumika ni mtindo wa lugha ya mtaani, jambo ambalo si zuri katika tafsiri. Mtindo wa lugha lengwa sharti ulingane na mtindo wa lugha chanzi.hivyo katika mfano huo, mtindo sahihi ungetakiwa kuwa;
Tafadhari! usijali! kama nitafika mapema, nitakusubiri.
Kusoma matini kwa mara ya mwisho
Jambo lingine la kuzingatia ni kuisoma upya matini chanzi. Katika kipengele hiki, mfasiri anashauriwa aisome matini chanzi kwa mara ya mwisho huku akipigia mstari au kuandika katika kidaftari kidogo msamiati, istilahi na misemo muhimu ya matini chanzi kama vile, methali, nahau maneno ya kitamaduni yasiyotafsirika, majina maalumu, n.k. kwa kupigia mstari au kuyaandika katika kidaftari kidogo ili iwe rahisi kwa mfasiri kuyatafutia visawe vyake kabla hata ya kuanza kutafsiri lakini pia kumsaidia mfasiri asiyasahau wakati wa kutafsiri.
Hayo ndiyo mambo ambayo, mfasiri anatakiwa kuyazingatia kabla hajaanza mchakato wa kutafsiri.
MAREJEO
Cartford [1995] A linguistic Theory Translation
Mwansoko, H.J.M na wenzake [2006] Kitangulizi cha Tafsiri, Nadharia na
Mbinu.TUKI.Dar-es-salaam
Newmark, P [1982] Approaches to Translation, Oxford, Pergamon Press
Newmark, P [1988] A Text book of Translation, London, Prentice Hall.
Oxford University Press Dar-es-salaam
Semzaba, E [2006] Ngoswe, Penzi Kitovu cha Uzembe. The General Booksellers LTD.
D.S.M
TUKI [2002] Kamusi ya Kiswahili Sanifu. TUKI, Dar-es-salaam
TUKI [1985] Kiswahili, Jarida la Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
www.bakita.org.tz retrieved on Monday 04th July 2018
www.jim-mission.org.uk retrieved on Monday, 04th July 2018
www.ajol.inf retrieved on Monday, 04th July 2018
Vitabu vilivyotafsiriwa ambavyo vimetumika kama marejeo
Ayi Kwei Armah, Wema Hawajazaliwa, kimetafsiriwa na Abdilatif Abdalla
Ferdinand Oyono: House boy, Kimetafsiriwa na Raphael Khasao na Nathan Mwele.
William Shakespeare: Juliasi Kaizari: Kimetafsiria na Julius K. Nyerere
Mabepari wa Venisi: Kimetafsiriwa na Julius K. Nyerere
Hekaya za Abunuwasi: Kimetafsiriwa na Interterritorial Language Committee, East Africa
Alfu Lela Ulela: Kimetafsiriwa na Sir Richard Burton
Sir Rider Haggard: Mashimo ya Mfalme Suleiman