UHUSIANO ULIOPO BAINA YA FONIMU NA ALOFONI

 Fonimu za lugha huweza kupata sura tofautitofauti kulingana na mazingira ambamo hutokea. Hii ina maana ya kwamba fonimu inaweza kubadilika ikachukua umbo moja kutokana na kutokea kwake katika mazingira fulani na ikaweza pia kubadilika ikachukua umbo jingine kutokana na kutokea kwake katika mazingira mengine tofauti. Hizi sura au maumbo mbalimbali ya fonimu moja hujulikana katika lugha ya kitaalamu kama alofoni.

1. Mitazamo juu ya Dhana ya Fonimu

Juhudi za kufasili dhana ya fonimu zilizofanywa wa wanaisimu mbalimbali zimezua mitazamo mbalimbali ya namna ya kuchambua dhana hii. Hadi sasa, mitazamo mitatu ifuatayo ndiyo hujulikana zaidi.

(i)        Fonimu ni Tukio la Kisaikolojia

Huu ni mtazamo uliokuzwa na kutetewa na wanasarufi geuzi-zalishi, mwanzilishi wake akiwa ni Noam Chomksy. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni dhana iliyo katika akili ya mzungumzaji wa lugha. Mtazamo huu unadai kuwa kila mzungumzaji wa lugha ana maarifa bubu ya idadi na jinsi ya kutamka fonimu za lugha yake. Chomsky anayaita maarifa haya kuwa ni umilisi (competence). Anadai kuwa maarifa haya ya fonimu hufanana kwa kiasi kikubwa miongoni mwa wazungumzaji wa lugha moja husika. Kinachotofautiana ni jinsi ya kudhihirisha (kutamka)  fonimu hizo, yaani utendi (perfomance). Chomsky anabainisha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuhitilafiana baina ya umilisi na utendi kutokana na matatizo mbalimbali ambayo mzungumzaji hukabiliana nayo. Matatizo hayo ni kama vile uchovu, ulemavu wa viungo vya matamshi, athari za mazingira, ulevi, na maradhi. Hivyo, kutokana na hali hii, fonimu hubaki kuwa tukio la kisaikolojia tu.

(ii)         Fonimu kama Tukio la Kifonetiki

Wafuasi wa mtazamo huu wanaongozwa na Daniel Jones. Daniel Jones anaiona fonimu kuwa ni [umbo] halisi linalojibainisha kwa sifa zake bainifu. Anadai kuwa fonimu huwakilisha umbo halisi la kifonetiki na inapotokea kukawa na fungu la sauti katika fonimu moja, sauti hizo huwa na sifa muhimu za kifonetiki zinazofanana. Hivyo, fonimu ya Kiswahili ni kitita cha sauti za msingi pamoja na alofoni zake.

(iii) Fonimu kama Tukio la Kifonolojia

Huu ni mtazamo wa kidhahania, ambapo huaminika kuwa fonimu ni kipashio cha kimfumo, yaani fonimu huwa na maana pale tu inapokuwa katika mfumo mahususi. Mwanzilishi wa mtazamo huu ni Nikolai Trubetzkoy. Yeye huamini kuwa fonimu ni dhana ya kiuamilifu na uamilifu huo hujitokeza tu fonimu husika inapokuwa katika mfumo wa sauti wa lugha husika. Kwa mujibu wa mtazamo huu, fonimu ni kipashio kinachobainisha maana ya neno. Mtazamo huu hutumia jozi sahili kudhihirisha dai lake. Mathalani, maneno baba na bata yana maana tofauti kwa sababu ya tofauti ya fonimu /b/ na /t/. Mtazamo huu hujulikana kuwa ni wa kifonolojia. Na kwa hakika, mawazo haya ndiyo yaliyoshika mizizi zaidi katika taaluma ya fonolojia na ndiyo inayofunzwa hivi sasa katika sehemu nyingi ulimwenguni.

Uhusiano kati ya Foni na Fonimu

Na.

Foni

Fonimu

1.

Hazina maana

Zina maana

2.

Ziko pekepeke

Zimo katika mfumo

3.

Nyingi

Chache

4.

Huweza kujitokeza kama alofoni

5.

Zinaponukuliwa, alama ya mabano mraba “[ ]” hutumika.

Zinaponukuliwa, alama ya mabano mshazari “/   /” hutumika

hati miliki zimehifadhiwa

Leave a Reply

scroll to top