uundaji wa maneno ni ujenzi au uzalishaji au utengenezaji wa maneno mapya. Uundaji wa maneno mapya husaidia kuongeza msamiati katika lugha ili kukidhi mahitaji ya mawasiliano. Uundaji wa maneno mapya husababishwa na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na maendeleo ya kisayansi yanayotokea katika jamii.
Uundaji wa msamiati mpya ni shughuli ambayo imekuwa ikiendelea tangu zamani, yaani kabla ya kuja kwa wageni, baada ya kuja kwa wageni na baada ya kupata Uhuru. Uundaji huo wa msamiati mpya ulifanyika katika viwango tofauti kulingana na nafasi ya Kiswahili katika maendeleo kwa nyakati hizo maalumu. Hata hivyo katika nyakati zote hizo, njia mbalimbali zimetumika. Litakuwa jambo jema kuzipitia njia hizo kwa ujumla na kuona taratibu zake na inapobidi kudokeza ubora na udhaifu wake na hatimaye kuona ni njia gani ni bora zaidi katika kukabiliana na kazi hii ngumu ambayo yawashughulisha sana wanalugha siku hizi katika kukiendeleza Kiswahili.
Zifuatazo ni mojawapo ya njia za uundajia wa maneno katika lugha ya Kiswahili:-
UTOHOZI:
Ni mbinu ambayo maneno kutoka lugha chanzi hutoholewa toka lugha chanzi na hatimaye hufanyiwa marekebisho kwa kufuata kaida au sheria za kifonolojia na kimofolojia za lugha pokezi kabla ya kutumiwa. Neno linapotoholewa hutamkwa na kuandikwa kwa utaratibu wa lugha pokezi, hata hivyo maana ya neno lililotoholewa hubakia ileile ya awali. Matinde, (2012 :114).
Mifano:
KIINGEREZA | KISWAHILI |
Switch | Swichi |
Lorry | Lori |
Budget | Bajeti |
Agenda | Ajenda |
Biology | Baolojia |
Dollar | Dola |
Oxygen | Oksijeni |
Ubora wa mbinu hii:
i) Mbinu hii ya utohozi ni mbinu rahisi ya kutumiwa katika uundaji wa msamiati. Mzungumzaji yeyote anaweza kutumia mbinu hii hata bila kuhudhuria kozi yoyote ya isimu au kufundishwa.
ii) Maneno mengi huweza kuundwa kwa kutumia mbinu hii ili kukidhi mahitaji ya matumizi katika lugha mbalimbali.
Udhaifu wa mbinu hii.
i) Mbinu hii hulemaza ubunifu wa wanajamii katika kuunda msamiati mpya wenye kuakisi utamaduni wa jamii husika.
ii) Lugha tohoaji huonekana kukosa uasilia yaani lugha huonekana kuwa chotara.
iii) Baadhi ya maneno katika Kiswahili ambayo yametoholewa kutoka lugha ya kiingereza katika lugha ya Kiswahili hutamkwa kwa namna tofauti kabisa.
Mifano;
KIINGEREZA | KISWAHILI |
Data | Data, deta |
Dance | Densi, dansi |
Bank | Bank, benki |
Radio | Redio, radio |
Hivyo basi, kutohoa maneno toka lugha nyingine ni ile hali ya lugha fulani kuchukua maneno toka lugha nyingine yaani kila lugha ina tabia ya kuchukua maneno toka lugha nyingine ili kukidhi mahitaji ya msamiati.
Maneno kutoka lugha nyingine yanapotoholewa hubadilishwa kimatamshi ili yafuate kanuni za lugha husika.
Katika lugha ya Kiswahili maneno yanayotoholewa hayana budi kusanifishwa na baraza la Kiswahili la Taifa ndipo yaruhusiwe kutumiwa rasmi.
2.KUBUNI
Njia ya pili ni ya kubuni. Njia hii yaweza kutumika kukabili mazingira ya aina mbili. Kwanza, kubuni msamiati ambao utataja mambo yaliyomo katika jamii ambayo hayajapata msamiati wa Kiswahili. Pili, kubuni msamiati ambao utataja mambo kutoka nje ya jamii yenye msamiati wa kigeni. Mara nyingi kukabili mazingira ya kwanza ni rahisi zaidi kuliko kukabili mazingira ya pili. Maingira ya pili yanaelekea kuwa magumu hasa kama Kiswahili kimechelewa kutoa msamiati wa Kiswahili. Mfano ikiwa jambo fulani na msamiati wake wa kigeni limeingia nchini tangu miaka ya sitini na kupewa msamiati wa Kiswahili miaka
ya themanini, ni dhahiri kuwa watumiaji watakuwa wamekwishazoea kutumia msamiati wa kigeni hivyo msamiati mpya wa Kiswahili, utachukua muda kukubalika na kutumiwa. Kwa njia kuu mbili za kubuni msamiati. Kuna kubuni kinasibu na kubuni kwa kuongozwa na vigezo maalumu.
Kubuni – Kinasibu
Katika njia hii, maneno mapya kabisa huundwa kwa kuzingatia kanuni za isimu za
lugha husika na kisha kuyapachika dhana mbalimbali. Kwa mfano mwanalugha anaweza kuunda
maneno “golo”, “kisopo” halafu akasema:
golo- solar system
Kisopo- radar
Watumiaji wa njia hii, wanadai kuwa njia hii itatatua tatizo la kuchukua maneno ambayo tayari yamo katika lugha na kuyashindilia mzigo mwingine. Wanaongeza kusema kwamba ni njia bora sana katika kuunda istilahi kwa vile istilahi hazitakiwi kubeba maana nyingi au vivuli vya maana. Pamoja na faida zilizotajwa hapo juu, wapo wanalugha ambao wanaipinga njia hii ya kubuni kinasibu. Wanadai kwamba katika kuunda msamiati mpya, ni bora kwa kiasi fulani pawepo na uhusiano baina ya kitaja na kitajwa katika msamiati ili kuleta mchomo fulani badala ya kuunda msamiati ambao hauna maana inayohusiana kabisa na dhana zinazotajwa. Mtaalamu wa lugha
Moc William, A. (1982) anasema kwamba, “…. nafikiri kwamba watu hawataki kupewa silabi. isiyo na maana. Wengi wetu wanapenda msingi wa neno fulani na maana yake utokane na msingi unaojulikana”. Kadhalika Mdee, J. (1981) anasema kuwa, wanaisimu wengine husita kuiafiki njia hii kwani inakiuka tabia ya asili ya uundaji wa maneno katika lugha. Kwa kawaida watumiaji wa lugha waliunda maneno ambayo yalikuwa na maana inayohusiana na dhana inayowakilishwa ama kimaumbile, kitabia au kimatumizi.
Kubuni kwa kutumia vigezo maalumu
Njia ya pili katika utaratibu wa kubuni ni ile ambayo mbunifu huongozwa na vigezofulani maalumu. Vigezo hivyo mara nyingi ni maumbile, tabia au matumizi ya kitu kinachotakiwa kiundiwe msamiati wa Kiswahili. Sifa hizi za msingi zinapururwa kutoka kwenye kitu kinachotakiwa kutajwa au kinachotajwa kwa msamiati wa kigeni na kisha kubuni msamiati utakaozingatia mojawapo ya sifa hizo kimaana. Mtaalamu mmoja Akida (1973) ameitumia njia hii katika kutunga msamiati wa muda wa sayansi. Mifano ya baadhi ya maneno
aliyobuni ni:
Abdomen( Fumbatio)Neno fumbatio limepatikana kwa kufata kazi yake; yaani kitu kama fuko ambamo ndani yake mnazuia vitu kama ini, nyongo, figo na kuacha juu pafu na moyo. Hivyo kitu hiki kimefumbatia vitu fulani ndani ya tumbo la kiumbe.
Antinomycets ( Uyogapele)Viyoga hivi husababisha mimea ya viazi kutoa miche au matunda yake yakiwa yameduduika kama yenye pele. Hasa ugonjwa wake huitwa pele za viazi, hivyo tumeona bora viyoga hivi viitwe viyoga vinavyoleta pele, ndipo tumenata neno “viyogapele”
Aerial roots and stems: (Mzizipau) Limetolewa neno “mzizipau” kwa sababu mizizi hii huning’inia tu si aghalabu kuota chini. Kwa hali hii tumeita mizizipau maana inaning’inia kama mapau ya nyumba
ambayo hayafiki ardhini bali hukaa juu juu.
Ukiangalia kwa undani njia hizi mbili za kubuni utaona kuwa njia hii ya pili haina upinzani mkubwa sana kwa vile msamiati unaopatikana una maana ambazo zina mfanano wa kiasi fulanina kile kinachotajwa na hivi kuibua hisia fulani kwa watumiaji. Maneno haya mara nyingi yaingiapo masikioni mwa watumiaji yaibua maana fulani vichwani mwao na hivi kuonekana ni maneno hai katika lugha. Mtaalamu wa lugha Hassani N. Moyo (Sept. 1983) anasema kwamba watu wengi wanalalamikia tafsiri za kubuni, wengine wanahisi tafsiri za kubuni zinazusha maneno mageni na magumu zaidi kuliko yale yanayofasiriwa. Je, Baraza (BAKITA) halina njia nyingine badala ya kubuni tafsiri?
TAFSIRI.
Matinde, (2012) anadai tafsiri ni mbinu ya kuunda maneno ambapo maneno au vifungu katika lugha chanzi hufasiriwa katika lugha lengwa. Ufasiri huu huzingatia muundo wa lugha pokezi.
Mifano,
KIINGEREZA | KISWAHILI |
Free market | Soko huria |
Ruling part | Chama tawala |
Ubora wa mbinu hii.
Mbinu hii huzingatia kigezo cha maana zaidi kuliko muundo wa maneno yaliyochukuliwa toka lugha chanzi na kutafsiriwa huafiki utamaduni wa lugha lengwa. Hali hii husaidia katika kuunda maneno yenye maana iliyo wazi na inayokubalika katika lugha lengwa.
Udhaifu wa mbinu hii.
Mara nyingi huwa vigumu kutafsiri baadhi ya manenotoka lugha chanzi kwa kufuata kigezo maana.
Kuna uwezekano wa kupata tafsiri ambazo hazina maana wala mantiki katika lugha lengwa.
Mfano.
Kitchen party – sherehe ya jikoni.
Things fall apart – vitu vilivyoanguka na kutapakaa.
Kuingiza maneno ya Kibantu na lahaja
Hii ni njia ambayo inapendekezwa na wanalugha mbalimbali. Hata hivyo kuna makundi mbalimbali ya watumiaji wa njia hii. Liko kundi la wale wapendeleao zaidi matumizi ya lahaja za Kiswahili na kundi la pili ni la wale wapendeleao zaidi lugha za Kibantu. Pamoja na mgawanyiko huu, wazo la msingi ni kwamba lahaja pamoja na lugha za Kibantu zinaweza kusaidia kuziba pengo la msamiati katika lugha ya Kiswahili japo kwa kiwango fulani tu.
Twasema kwa kiwango fulani tu kwa vile imethibitika katika uchunguzi wa istilahi za migomba kuwa wakulima wa migomba wamefanikiwa kuainisha idadi kubwa ya migomba na mazao yake kujenga istilahi nyingi za kutumia katika kushughulikia kazi ya kilimo hiki. Kwa bahati mbaya maneno yaliofanikiwa kutengwa hayaendi zaidi ya elimu ya ujuzi wa kawaida. Msamiati uliojitokeza hauwezi kwa mfano kusaidia kujaza pengo la msamiati wa botani au kemia katika taaluma ya Sayansi (Khamisi 1980).
Hata hivyo utaratibu uliowekwa na BAKITA ni kwamba baada ya kukosa msamiati wa Kiswahili, kwanza unatalii lahaja za Kiswahili ndipo ifuatwe na Kibantu halafu Kiarabu na mwishowe Kiingereza. Utaratibu huu uliopendekezwa na BAKITA haujafuatwa ipasavyo. Ukweli huu unathibitishwa na kauli ya Kimani (1983) Mtaalamu wa Kiswahili kutoka Kenya kwamba, baadhi ya watu nchini Kenya wametoa hoja kwamba Kenya ina maneno zaidi ya 5,000 ya asili ambayo yanaweza kutumiwa katika kubuni maneno mapya badala ya kuchukua maneno yaliyobuniwa na Tanzania. Kwa kweli kauli hii ni changamoto kubwa sana kwa wale wote wanaohusika katika zoezi hili la kuunda msamiati mpya.
Mifano michache ya njia hii kutoka Kamusi la BAKITA Na. 3 itasaidia kupata picha halisi
Close season. – sango (Kingoni)
cut worm – sota (Kijita)
leaf minor – kidomozi (Kibondei)
foot and mouth disease -Shuna (Kisumbwa, Haya)
weevils -fukuzi (KIngoni, Kibondei, Kijita)
leaf curl – ngozi (Kimtang’ata)
new castle – mdondo (Bara)
Kama tulivyokwisha ona hapo juu ni kwamba njia hii ni nzuri na maneno yake yaweza kupokelewa kwa urahisi na watumiaji. Hata hivyo njia hii ina kikomo chake kwa vile ni kweli kwamba lahaja na lugha za Kibantu hazijapanuka kimsamiati, katika taaluma za Sayansi, elimu siasa, uchumi, teknolojia na kadhalika kiasi cha kutosha kumeza maendeleo ya kisasa yaliofikiwa. Kwa mfano ni lahaja gani au lugha gani ya Kibantu ina msamiati wa bomb, nuclear, video, electrone, combine harvester, television, na vitu vingine kama hivi? Jibu ni dhahiri kuwa hakuna. Kama hivyo ndivyo basi ni dhahiri kuwa hii sio njia pekee ya
kutegemewa. Lazima pawepo na njia nyingine ambazo zitasaidiana na njia hii.
Kuhamisha maana
Hii ni njia ambayo neno fulani la Kiswahili hupewa maana mpya katika matumizi. Uchaguzi wa maneno haya sio wa kiholela au kibahati nasibu; maneno yachaguliwayo huibua fikra au dhana fulani.
Mifano michache ya maneno ya aina hii ni kama ifuatavyo:
Neno KUPE lina maana ya Mdudu agandaye mwilini nakufyonza damu ya wanyama kutokana na dhana hii neno hili linatupa maana mpya ya Mnyonyaji Mnyonyaji. Mtu aishie kwa jasho la
wengine
Neno TAWI lina maana yaSehemu ya mti inayobeba majani na matunda. kutokana na neno hili tunapata maana nyine mpya ambayo ni Sehemu ndogo ya Chama au Shirika
Baadhi ya wanalugha hawaungi mkono njia hii hasa inapotumika katika kuunda istilahi. Dai lao
ni kwamba istilahi hazitakiwi kuwa na vivuli vya maana na zaidi ya hayo utaptibu huu unayabebesha maneno mizigo mikubwa ya maana. Kurakabu, kufupisha, kunyambulisha na takriri
Hii ni njia ambayo unapanga maneno mawili au zaidi ili kuunda neno jipya lenye maana moja.
Mfano Katibu Kata, Katibu muhtasi, nguvu kazi, mpiga makasia, kidakatonge n.k.
Kufupisha
Hii ni njia nyingine ya kuunda maneno. Kuna vifupisho ya aina mbili kuu. Kuna
vifupisho akronimu na vifupisho mchanganyo (blending)
Rubanza (1996) anaeleza kuwa baadhi ya majina ya maneno katika lugha nyingine za dunia hutokana na ufupishaji wa maneno yanavyotumiwa kwa pamoja kwa kutumia herufi au silabi za mwanzo tu za maneno hayo. Njia hii ameita Akronimu.
Matinde (2012) anaeleza kuwa ufupishaji ni mbinu ambayo hutokana na kitenzi ‘fupisha’ chenye maana ya kufanya kitu kiwe kifupi au kupunguza urefu wa kitu.
Kwa mujibu wa Rubanza (1996) njia ya ufupishaji imegawanyika katika sehemu kuu mbili kama ifuatavyo:-
Vifupisho akronimu
Haya ni maneno yanayopatikana kwa kuunganisha sehemu ya kwanza au ya mwisho ya
maneno mawili au zaidi.
Mfano:
UKIMWI – Ukosefu wa Kinga Mwilini.
TUKI – Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
BAKITA – Baraza la Kiswahili Tanzania.
Vifupisho mchanganyiko
Haya ni maneno yanayopatikana kwa kuunga maneno mawili na kuwa moja. Kwa
kawaida sehemu ya mwanzo ya neno la kwanza huungwa na sehemu ya mwisho ya neno la pili.
Kwa mfano;
Insecticide (Kiua + wadudu) = Kiuadudu
Aphid inaitwa (Kiduri + sukari )= Kidukari
Uhurutishaji.
Uhurutishaji ni tendo jingine linalokaribiana na tendo la akronimi, katika tendo hili vijisehemu vya maneno huwekwa pamoja kuunda neno jipya. Mfano katika lugha ya Kiswahili tunaweza kupata maneno kama vile:-
Chakula cha jioni – Chajio.
Hati za kukataza – Hataza.
Mama mdogo – Mamdo.
Chakula cha mchana – Chamcha.
Vijisehemu vilivyowekwa pamoja si lazima viwe vyanzo vya maneno.
c. Ufupishaji Mkato (clipping).
Matinde, (2012) anatofautiana na Rubanza (1996) kwa kuongeza mbinu nyingine ya ufupishaji ambayo ni ufupisho mkato (clipping). Katika mbinu hii baadhi ya vipashio au silabi hudondoshwa na kuacha sehemu tu ya neno asilia.
Mifano.
NENO ASILIA | KIFUPISHO |
Dar es salaam | Dar |
Shemeji | Shem |
Morogoro | Moro |
Dada | Da |
Binamu | Bina |
Marejeo
Akida, H. 1973. “Msamiati wa muda wa Sayansi” katika Kis wahil i vol. 43/2.
Akida, H. 1976. “Misingi ya Uimarishaji wa Kazh za Istilahi Kimataifa”. DSM, Makala
isiyochapishwa.
BAKITA, Kamusi Na. 3: Magonjwa ya mifugo, mimea na WEIdudu waharibifu, DSM.
Gibbe, A.G. 1978. “Macadeleo ya Istilahi za Kiswahili”. DSM, Maka la isiyochapishwa.
Khamisi, A.M. 19880. “Kujenga Kiswahili kwa kutumia lugha za Kibantu”. DSM, Makala
isiyochapislhwa.
MacWilliam, A. 1982. “Maoni kuhusu tafsiri ya istahi za Sayansi”. DSM, Makala
isiyochapishwa.
Mdee, J.S. 1981. “Uundaji wa istilahi kwa kategemea lugha husika” DSM, Makala
isiyochapishwa.
- “Matatizo ya kuunda istilab kanma yanavyojitokeza katika Kiswahili”. DSM,
Makala isiyochapishwa. - Stageberg, N.C. 1971. “Six processes of word formation” kstika an Introducto ry Engiish
Grammanr. New York: Rinehazt and Winston INC.