Viambishi Awali
Viambishi awali Hivi hupachikwa kabla ya mzizi wa neno na huwa ni vya aina tisa:-
i. Viambisha awali vya nafsi– hivi hudokeza upatanishi wa nafsi katika kitenzi, zipo nafsi tatu, nafsi ya kwanza, ya pili, na ya tatu na viambishi vifuatavyo huwakilisha nafsi hizi:
Nafsi | Umoja | Uwingi |
Ya kwanza | Ni- | Tu- |
Ya pili | U- | M- |
Ya tatu | A- | Wa- |
Mfano katika neno :
Nafsi | Umoja | Uwingi |
Ya kwanza | Ni-nasoma | Tu-nasoma |
Ya pili | U-nasoma | M-nasoma |
Ya tatu | A-nasoma | Wa-nasoma |
ii. Viambishi awali vya ngeli– hivi hupatikana mwanzoni mwa nomino au vivumishi ili kudokeza hali ya umoja na uwingi.
Mfano:-Mtu (umoja) – Watu (uwingi)
Msafi (umoja) – Wasafi (uwingi)
iii. Viambishi awali vya ukanushi – hivi hudokeza hali ya uhasi wa tendo. Huwakilishwa na mofimu (ha-) na (si-)
Mfano:- Amekula (uyakinifu) – Hajala (ukanushi), Nakula (uyakinifu) – Sili (ukanushi)
iv. Viambishi awali vya Njeo- hivi hudokeza nyakati mbalimbali ambazo ni wakati uliopita, uliopo na ujao.
Nyakati | Mofimu |
Uliopo | Na- |
Ujao | Ta- |
Uliopita | Li- |
Mfano:- Mlituona
Utakuja
v. Viambishi awali vya hali- hivi hudokeza hali mbili za nyakati ambazo ni mazoea ambayo huwakilishwa na mofimu {hu} na timilifu inayowakilishwa na mofimu {me}.
Mfano:-Hucheza
Amelima
vi. Viambishi awali vya masharti – Hivi hudokeza hali ya masharti au uwezekano katika tendo. Mofimu hizo ni kama –ki-, nge-, ngali- n.k.
Mfano:- ukija
Ungekuja
Angalimkuta
vii. Kiambishi cha urejeshi wa mtenda (kiima) – Hiki hudokeza urejeshi wa nomino inayotenda katika kitenzi.
Mfano: – Aliyekuja {-ye-} hudokeza urejeshi wa mtenda.
viii. Kiambishi kiwakilishi cha mtendwa au mtendewa (shamirisho) – hivi huwakilisha mtendwa au mtendewa wa jambo.
Mfano; Nilimpiga, Uliukata, Nimeipenda, Wameniteta.
ix. Kiambishi awali cha kujirejea (kujitendea) – hiki huwakilishwa na mofimu (-ji-)
Mfano; kujipenda