Vitate

Vitate ni maneno ambayo katika matamshi yake yanakaribiana lakini maana ni tofauti.   Angalia mifano ifuatayo;                                                                                                                                                          

Tata

  1. hali ya kutoeleweka
  • sentensi hii ni tata.
  1. fundo katika uzi
  • uzi umeingia tata/umetata. 

Dada

  1. ndugu wa kike

Tua

  1. shuka kutoka angani
    • ndege ilitua uwanjani.
  2. weka chini k.v. mzigo

Dua

  1. maombi kwa Mungu
  • omba dua
  • piga dua –apiza/laani

Toa

  1. ondoa kitu ndani ya kinginea
  2. kinyume cha jumlisha

Doa

  1. alama yenye rangi tofauti  na mwili wa kitu
  2. dosari/ila/walakini

Ndoa

  1. arusi/makubaliano rasmi ya mwanamke na mwanamume kuishi pamoja kama mke na mume/chuo

Tundu

  1. uwazi mdogo wa mviringo kwenye kitu k.v. sindano
  2. kitu maalum cha kuwekea ndege kilichotengenezwa kwa mabati, matete n.k.

Dundu

  1. mdudu anayebeba uchafu
  2. rundo la vitu /mtumba

Tuma

  1. peleka kitu k.v. barua kwa njia ya posta
  2. agiza mtu kufanya jambo

Duma

  1. mnyama mkubwa mwenye umbo kama la paka
  2. kamata, hasa katika vita

K/G                                    

Kuku 

  1. aina ya ndege anayefugwa nyumbani

Gugu

  1. mmea unaoota mahali usipotakiwa
  2. mmea wa mwituni mfano wa unyasi

Kuni

  1. vipande vya  mti vya kukokea moto

Guni

  1. shairi la arudhi lililokosa kutosheleza kanuni moja au zaidi ya uandishi

Kuna

  1. kwaruza kwa kucha /kitu chenye menomeno

Guna

  1. toa sauti ya kuonyesha kukataa, kutoridhika, au kuchukia jambo.

Kenge

  1. mnyama kama mjusi mdogo

Genge

  1. kundi la watu 
  2. pango/shimo

Kesi

  1. Daawa/mashtaka yanayosikilizwa mahakamani

Gesi

  1. hewa inayotumiwa kupikia au kutiwa katika vinywaji
  2. hewa ambayo haigeuki na kuwa majimaji katika joto la kawaida

CH/J

Changa

  1. toa kitu ili kukusanya kwa kusudi fulani
  2. siokomaa
  3. chanja/pasua vipande vipande vidogo vidogo k.v. kuni

Janga

  1. hatari/balaa

Chema

  1. kizuri

Jema

  1. zuri

Chini

  1. kwenye ardhi/sakafu

Jini

  1. shetani/ mtu muovu

Choka

  1. pungukiwa na nguvu baada ya kufanya kazi

Joka

  1. nyoka mkubwa sana

Chungu

  1. chombo kinachofinyangwa cha kupikia
  2. kinyume cha tamu
  3. idadi kubwa (chungu nzima)
  4. mdudu mdogo wa jamii ya siafu

Chambo

  1. kinachowekwa kwenye mtego kunasia wanyama,samaki n.k.

Jambo

  1. habari,tukio shughuli

Kucha

  1. elekea asubuhi
  2. ogopa

Kuja

  1. hali ya kusogea karibu

Chuma

  1. pata mali
  2. madini magumu yanayotumiwa kujengea na kuundia vitu
  3. tungua matunda au maua kutoka mtini

Juma

  1. wiki
  2. jina la mtu

Chenga

  1. hepa kwa hila
  2. mchele uliovunjikavunjika(mchele wa chenga)

Jenga

  1. aka nyumba
  2. fanya madhubuti/imarisha

Mchi

  1. mti wa kupondea kwenye kinu

Mji

  1. makazi ya watu wengi kulikojengwa nyumba nyingi
  2. mahali kaburini anapowekwa mauti
  3. sehemu ya kati ya chupa ya mwanamke mja mzito inayounganisha mtoto na           mwili wa mama

Kichana

  1. kitu cha kuchania nywele

Kijana

  1. mtu wa makamo mwenye nguvu/mtoto wa kiume kabla ya kubaleghe

F/V

Faa

  1. kusaidia
  2. kuwa vizuri

Vaa

  1. eneza kitu katika mwili ili kufunika sehemu fulani

Fua

  1. safisha nguo
  2. tengeneza kitu kutokana na madini
  3. toa maji katika chombo
    • fua maji
  4. Hakufua dafu. (hakufaulu)

Vua

  1. pata samaki kwa kutumia wavu, mshipi, ndoana n.k.
  2. ondoa nguo mwilini
  3. nusuru, okoa, ponya
  4. vua macho (tazama)

Fika

  1. wasili mahali
  2. bila shaka/kabisa

Vika

  1. valisha

Fuka

  1. toa moshi bila kuwaka
  2. uji wowote mwepesi (uji fuka)

Vuka

  1. enda upande wa pili

Fuma

  1. piga kwa mkuki
  2. ona kwa ghafla bila kutazamia mtu anayetenda jambo ovu
  3. tengeneza kitu kwa kusokota nyuzi,ukindu n.k

Vuma

  1. julikana kwa watu wengi k.v. habari, mtu n.k.
  2. toa sauti nzito  k.v. simba,.upepo mkali,.ngoma n.k.

Afya

  1. hali nzuri ya mwili/siha

Avya

  1. toa mamba
  2. tumia ovyoovyo mali, pesa, n.k.

Fito

  1. vipande vya miti au chuma vya kujengea nyumba

Vito

  1. mawe ya thamani

Fuja

  1. tumia vibaya
  2. haribu mali, nguo ,chakula n.k.

Vuja

  1. pita kwa kitu mahali penye upenyo
    • Gunia hili linavuja.

Vunja

  1. fanya kitu kigumu kuwa vipande vipande
  2. badilisha pesa ziwe ndogondogo
  3. enda kinyume na kanuni

Futa

  1. pangusa
  2. chomoa kisu
  3. toa maji nje ya chombo/fua maji

Vuta

  1. fanya kufuata/burura
  2. ingiza hewa au moshi mapafuni

Wafu

  1. waliokufa

Wavu

  1. utando wa nyuzi wa kufulia samaki,kutegea wanyama,kuweka golini/kimiani n.k

CH/SH

Chaka

  1. mahali penye miti iliyosongamana
  2. msimu wa kaskasi/joto na ukavu wa ardhi

Shaka

  1. wasiwasi
  2. tuhumuma 

Chali

  1. lala mgongo juu kichwa chini
  2. mtu anayechekesha watu kwa kuwatolea mkasa

Shali

  1. kitambaa cha begani cha shehe

Shari

  1. balaa (pata shari)

Chati

  1. mchoro unaotoa maelezo Fulani

Shati

  1. vazi la juu la mwili lenye mikono

Sharti

  1. lazima

Choka

  1. pungukiwa na nguvu baada ya kufanya jambo kwa muda mrefu

Shoka

  1. kifaa cha kukatia na kupasulia miti

Chombo

  1. ala ya kufanyia kazi

Shombo

  1. harufu mbaya ya samaki

Chokoa

  1. tia kitu chenye ncha kwenye tundu au shimo ili kutoa kitu k.m chokoa meno

Shokoa

  1. kazi ya kulazimishwa (fanyishwa shokoa)
  2. shamba lililolimwa na kuachwa kumea nyasi

TH /DH

Thamini

  1. tia maanani, heshimu

Dhamini

  1. toa pesa maakamani ili mshtakiwa asitiwe korokoroni

Thamani 

  1. kima

Dhamana

  1. malipo ya kortini

Thibiti

  1. kuwa ya kweli/kuaminika
  2. Habari imethibiti.

Dhibiti

  1. tia mkononi
  2. Nikidhibiti pesa zangu kutoka kwake nitanunua baiskeli.
  3. weka chini ya mamlaka

Ridhi

  1. kubali
  2. pendezwa na jambo

Rithi

  1. miliki kitu kutoka kwa mtu aliyekufa ama uliye na uhusiano naye
  2. pata jambo au ujuzi kutoka kwa mtu mwingine

A/H

Apa

  1. tamka jina aghalabu la Mungu kuthibitisha jambo Fulani

Hapa

  1. mahali karibu

Ama

  1. au

Hama

  1. toka mahali fulani ili kwenda mahali pengine kuishi (gura)

Adimu

  1. -a shida kupatikana,nadra

Hadimu

  1. -mtumishi (mahadimu)

Ajali

jambo la madhara au hatari

Hajali

  1. kinyume cha jali

Auni

  1. saidia

Launi

  1. rangi

L/R

Lahani

  1. tuni

Rahani

  1. chumba maalum katika nyumba au chombo cha kuwekea vitu

Lea

  1. tunza mtoto

Rea

  1. ghadhibika

Lemba

  1. nyanganya kwa hila,punja

Remba

  1. pamba, rembesha

Fahali

  1. ng`ombe dume

Fahari

  1. -a kujivuniwa kwa watu

Mahali

  1. sehemu ambapo mtu au kitu huweza kukaa

Mahari

  1. mali au fedha inayotolewa na mwanamme kupewa wazazi wa mwanamke anayetaka kumuoa

S /SH

Saba

  1. namba inayoonyesha idadi

Shaba

  1. madini yenye rangi ya manjano

Saka

  1. tafuta,winda

Shaka

  1. wasiwasi
  2. tuhuma
  3. kutokuwa na hakika

Suka

  1. tikisa kitu
  2. pitisha kitu kama nywele baina ya zenyewe kupata mfumo fulani

Shuka

  1. enda chini kutoka juu ya kitu
  2. kitambaa cha kujifunga kiunoni

Soga

  1. mazungumzo ya kupitisha wakati

Shoga

  1. jina waitanalo wanawake marafiki
  2. msenge

Sababu

  1. kinachofanya jambo kutokea,chanzo

Shababu

  1. kijana

 J/NJ

Jaa

  1. tosha
  2. tapakaa kila mahali
  3. mahali pa kutupia taka

Njaa

  1. hali ya tumbo kutaka kupata chakula
  2. ukosefu mkubwa wa chakula

Chema

  1. kizuri

Jema

  1. zuri

Njema

  1. nzuri

Jia

  1. sogelea karibu

Njia

  1. barabara
  2. namna au jinsi ya kufanya jambo

Jozi

  1. vitu viwili vinavyofanana vilivyo pamoja

Njozi

  1. maono yatokeayo usingizini;ruia

Jana

  1. siku kabla ya leo,mwaka kabla ya huu
  2. buu la nyuki-kama kiluwiwi cha nzi

Njana-samaki mwenye rangi nyekundu

D/ND

Dege

  1. eropleni kubwa
  2. ndege mkubwa
  3. ugonjwa wa watoto unaosababishwa na homa kali

Ndege

  1. mnyama aghalabu anayeruka kwa mabawa
  2. eropleni inayosafiri angani
  3. ndege mbaya/mzuri (bahati nzuri/mbaya)

Duni

  1. kitu chenye thamani ya chini

Nduni

  1. ajabu/lisilo la kawaida

B/MB

Basi

  1. gari la abiria
  2. kisha

Mbasi

rafiki

Buni

  1. gundua
  2. unda
  3. tunga

Mbuni

  1. ndege asiyeweza kuruka lakini huenda mbio sana
  2. mkahawa au mti uzaao kahawa

Bali

  1. lakini
  2. sijali wala sibali (kusisitiza kutojali)

Mbali

  1. si karibu
  2. tofauti

Mbari

  1. ukoo

Bega

  1. sehemu ya mwili juu ya mkono na chini ya shingo

Mbega

  1. nyani
  2. manyoya ya ndege wanayojifunga wachezaji ngoma (jifunga mbega)

Iba

  1. chukua kitu cha mtu mwingine bila ruhusa

Imba

  1. tamka maneno kwa sauti ya mziki

G/NG

Gawa

  1. tenga katika sehemu mbalimbali
  2. aina ya ndege wa usiku;kirukanjia

Ngawa

  1. mnyama afananaye na paka

Guu

  1. mguu mkubwa sana

Nguu

  1. kilele cha mlima
  2. nguru_aina ya samaki

Goma

  1. kataa kufanya jambo mpaka masharti fulani yatimizwe
  2. ngoma kubwa sana
  3. duwi (aina ya samaki)

Ngoma

  1. ala ya mziki inayotengenezwa kwa kuwambwa ngozi kwenye mzinga (piga ngoma)
  2. mchezo wa kufuata mdundo wa ngoma (cheza ngoma)

Koma

  1. alama ya kituo
  2. acha kufanya jambo

P/B

Pata

  1. kuwa na jambo, hali au kitu
  2. kuwa kali
  • Kinolewacho hupata.

Bata

  1. ndege mwenye vidole vilivyotandwa aghalabu akaaye majini

Papa

  1. samaki mkubwa

Baba

  1. mzazi wa kiume

Pana

  1. kinyume cha –embamba

Bana

  1. finya

Bango

  1. uwazi ulio ardhini,mtini au jabalini

Bango

  1. kipande cha karatasi ngumu kama kadi
  2. bati linalozuia matope juu ya gurudumu la gari au baiskeli

Pacha

  1. watoto wanaozaliwa kutokana na mamba moja

Bacha

  1. tundu kwenye ukuta; shubaka(closet)

Paja

  1. sehemu ya mguu kati ya goti na nyonga

Pania

  1. kazana ili kufanya jambo lililokusudiwa

Bania

  1. zuia kitu bila ya kutaka kukitumia (bania pesa)

Pima

  1. tafuta urefu, uzito n.k.

Bima

  1. mkataba na shirika wa kulipa pesa ili kupata fidia mtu anapofikwa na hasara

Punda

  1. mnyama

Bunda

  1. fungu la karatasi,noti,ngozi n.k

Panda

  1. enda juu
  2. kifaa cha kurushia vijiwe; manati
  3. baragumu
  4. tia mbegu ardhini ili zimee

Banda

jengo kubwa la kuwekea vitu au wanyama

Pasi

  1. fuzu/faulu
  2. hati inayomruhusu mtu kusafiri nje ya nchi/pasipoti
  3. chombo cha kunyooshea nguo

Basi

  1. gari kubwa la abiria

Mbasi

  1. rafiki

T/D

Tamu

  1. enye ladha ya kuridhisha mdomo

Damu

  1. maji mekundu yanayozunguka mwilini
  2. ukoo

Taka

  1. kuwa na haja ya jambo fulani
  2. uchafu

Daka

  1. pokea kwa mikono kilichorushwa
  2. tunda bichi (nazi daka/danga)

Tokeza

  1. fanya kuonekana

Dokeza

  1. toa habari za siri kwa uchache

Tai

  1. ndege mkubwa mwenye makucha marefu alaye mizoga (vulture)
  2. kitambaa kinachovaliwa kwenye ukosi wa shati

Dai

  1. taka kupewa kilicho chako
  2. habari inayosemwa na haijathibitishwa

K/G

Kamba

  1. uzi mnene
  2. samaki mdogo
  3. mnyama wa baharini mwenye miguu mingi ambaye huliwa
  4. kata kamba (kimbia)

Gamba

  1. ngozi kama pembe ya kasa, samaki ,kasa au kobe(scales)

Konga

  1. kuwa mzee
  2. kusanya vitu au watu mahali pamoja (kongamano)
  3. meza maji kidogo ili kupunguza kiu (konga roho)

Gonga

  1. kutanisha kitu kimoja na kingine kwa kuvipiganisha

Koti

  1. vazi zito livaliwalo juu ya nguo

Korti

  1. mahakama

Goti

  1. kiungo cha mguu kinachounganisha paja na muundi

Mfugo

  1. mnyama anayefugwa nyumbani kwa ajili ya kuliwa au biashara

Mfuko

  1. kitu cha kitambaa cha kutilia vitu

Tegua

  1. fanya mtego usifanye kazi
  2. ondoa chombo kama chungu mekoni
  3. fanya kiungo cha mwili kifyatuke

 Tekua

  1. angusha kwa kusukuma
  2. ng`oa kwa nguvu k.v. mmea

Mkuu

  1. kiongozi
  2. wenye hadhi kubwa

Mguu

  1. kiungo cha binadamu au mnyama cha kusimamia au kutembelea

Oka

  1. tia ndani ya tanuu kitu ili kiive au kikauke k.v unga uliokandwa au matofali

Oga

  1. safisha mwili
  2. enye hofu

Pika

  1. weka kitu k.v. chakula sufuriani juu ya moto ili kiive

Piga

  1. kutanisha vitu kwa nguvu
  2. piga chafya, maji, hodi n.k.

Ukali

  1. hali ya kutokuwa mpole 
  2. hali ya uchungu (ladha)

Ugali

  1. chakula kinachopikwa kwa unga wa mahindi na kusongwa na maji moto hadi yakauke

Leave a Reply

scroll to top