Sifa za lugha

Lugha huwa na sifa fulani za kimsingi ambazo zinapatikana katika lugha zote,  nazo ni ::

  • Lugha huzaliwa –  lugha  inaweza chipuka kwa mara ya kwanza, au msamiati mpya huweza kuzuka katika lugha ambazo zimekomaa kama vile kiswahili kuwakilisha dhana ambazo ni geni ,maneno haya  mapya huunda au kubuniwa  kwa kutumia mbinu mbalimbali na yakatumika katika kiswahili kuwakilisha dhana jhizo geni.
  • Lugha hukua – Lugha hukua kuambatana na maendeleo na mabadiliko mbalimbali katika mazingira yake.
  • Lugha inaweza kufa – Huu ni wakati ambapo lugha hudidimia na kukoma kutimiza dhima yake miongoni mwa wanajamii.ama msamiati flani wa lugha kukosa kutumika na kupotea kabisa.
  • Kila lugha ina sifa zake- lugha zote huwa na sifa zake bainifu ambazo huitambulisha 
  • Lugha huweza kuathiri na kuathiriwa – Ni muhimu kufahamu kwamba lugha yoyote ile inaweza ikaathiri utaratibu wa lugha nyingine katika kiwango fulani au viwango vyote vya lugha.
  • Lugha ni mali ya jamii –  Lugha haiwezi milikiwa na mtu binafsi, lugha huwa ni mali ya jamii inayoitumia lugha husika katika mawasiliano.
  • Lugha hubadilika – Lugha yoyote ile hupitia mchakato wa mabadiliko kutoka na mpito wa wakati, mazingira, maendeleo katika nyanja ya teknolojia, habari na mawasiliano.

                Mabadiliko katika lugha huweza kujitokeza kwa njia zifuatazo:

  • Kifonolojia – Mabadiliko kifonolojia yanahusisha kubadilika kwa kanuni na mfumo wa matamshi katika lugha husika.Aghalabu, mabadiliko hayo hutokana mtindo wa lugha kukopa misamiati iliyo na sauti zisizopatikana katika lugha asilia ikiwemo mabadiliko mengineyo.
  • Kimofolojia – Mabadiliko kimofolojia hutokea wakati utaratibu wa lugha kimaumbo unapobadilika hasa kuhusiana na kanuni za uundaji wa maneno.
  • Kisemantiki na kileksia – Mabadiliko haya hujitokeza katika maana au leksimu ya lugha husika.
  • Kuongezeka kwa leksimu hutokana na mbinu au njia zote za uundaji wa maneno.Leksimu inapoongezeka maana huongezeka vilevile kwa sababu huambatana na dhana inayowakilishwa.
  • Kisintaksia – Mabadiliko ya lugha kisintaksia husababisha utaratibu wa lugha ulio tofauti na ule wa awali.
  • Kila lugha ya mwanadamu imeundwa katika mifumo miwili mikuu; mfumo wa sauti na mfumo wa maana. Lugha huundwa kwa sauti ambazo huunganishwa kuunda neno au sehemu ya neno, maneno nayo huungana kuunda miundo mikubwa zaidi yenye maana kama virai, vishazi, sentensi na aya.Katika muunganiko huu wa maneno na miundo mbali mbali, huwa kuna kanuni na sheria zinazodhibiti mfuatano wa kila kipashio. Kuna kanuni zinazodhibiti mfuatano wa sauti, mfuatano wa mofimu, mfuatano wa maneno na hata mfuatano wa sentensi.
  • Lugha ni mfumo wa sauti nasibu

Lugha ni ya nasibu kwa maana kwamba, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya neno  na kitu chenyewe tunachotumia katika ujenzi na matumizi mengine. Hii ina maana kwamba, maumbo ya ishara za kiisimu hayana uhusiano wowote au mfanano wowote na maana ambazo tunayapa. Kwa mfano neno “kitabu” hakuna watu walikaa na kusema kuanzia leo hiki kitaitwa kitabu. Vile vile hakuna uhusiano wowote kati ya neno “kitabu” na umbo linalorejelewa. Uhusiano wake ni wa nasibu tu na hutofautiana kutoka  lugha moja na nyingine. 

  • Lugha ni maalumu kwa mwanadamu

Lugha ni chombo cha mawasiliano ambacho amejaliwa binadamu tu na kwamba hakuna kiumbe mwingine ambaye si binadamu mwenye uwezo wa kuzungumza na kutumia lugha. Hii ina maana kuwa kuna sifa fulani za lugha za binadamu ambazo hazipatikani kwa kiumbe mwingine yeyote yule isipokuwa mwanadamu. Ingawa ndege, mbwa, nyuki, tumbili wanaweza kuwasiliana, mawasiliano yao huwa ni ya sauti au ishara ambazo kimsingi siyo lugha, pia huwa yanadhibitiwa na hisia tu kama hofu, njaa, na ishara za kutoa taarifa. Binadamu ana uwezo wa kujifunza lugha mbalimbali na kuitumia katika mazingira yake na kitu ambacho wanyama hawawezi. Kwa mfano, ukimchukua mbwa wa marekani na kumleta Kenya atatoa sauti ile ile sawa na mbwa wa Kenya kwa kueleza shida ile ile au kutoa ishara ile ile.

  • Lugha ni mfumo wa ishara

Uishara wa lugha unamaanisha kuwa maneno huambatanishwa au huhusishwa na vitu, matendo,mawazo au hisia kwa makubaliano ya unasibu tu. Vile vile, yale tunayoyasoma katika maandishi ni ishara tu, maana zake lazima zipatikane katika muktadha wa mawasiliano. Hivyo basi, tunapojifunza lugha lazima tufahamu mfumo wa alama za lugha hiyo na kuelewa uhusiano uliopo kati ya ishara na vitu vinavyowakilishwa.

  • Lugha hutumia sauti

Sifa kuu ya lugha ni kutumia sauti ambazo hutengenezwa na ala za sauti. Pamoja na maendeleo ambayo mwanadamu ameyafikia kwa sasa katika uandishi na uwasilishaji wa taarifa kwa kutumia lugha sauti ndiyo msingi wa kila kitu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba:

  1. Mtoto hujifunza kuzungumza kabla hajajifunza kusoma na kuandika.
  2. Mtoto hujifunza lugha moja kwa moja bila kufikiri kadiri anavyokuwa
  3. Maandishi yalikuja baada ya mazungumzo
  4. Maandishi huwasilisha yale yanayozungumzwa
  5. Watu kwa kawaida hutumia muda mwingi kuzungumza kuliko kuandika

Kuna mambo mengi ya muhimu katika sauti za lugha ambayo hayawezi kuwasilishwa vema kwa kutumia maandishi. Mambo hayo ni kama, kiimbo, toni, mkazo, kidatu; haya ni muhimu katika mawasiliano lakini hayawezi kuwasilishwa kisawasawa kwa kutumia maandishi

  • Lugha ni kwa ajili ya mawasiliano

Kwa kutumia lugha binadamu anaweza kufanya vitu ambavyo viumbe wengine hawawezi kuvifanya. Vile vile lugha hutuwezesha sisi kuzungumzia hisia zetu, matamanio yetu, kucheza, kufanya kazi n.k. Yote haya yanawezekana kwakuwa tunayo lugha ambayo ndiyo nyenzo kuu ya mawasiliano.

  • Lugha zote ni sawa – hamna lugha iliyo bora zaidi ya zingine
  • Mfumo wa Lugha

Hoja kuwa lugha ni mfumo inamaanisha kuwa lugha ina muundo unaohusisha viambajengo mbalimbali. Viambajengo au vipashio hivi ni sauti, neno na sentensi. Kwa pamoja, vipashio hivi hushirikiana kuunda tungo zenye maana na kama tungo hizo hazina maana au kama haziwasilishi ujumbe wowote basi tunasema haziwi lugha.

Leave a Reply

scroll to top